Hoteli ya Bwawani, moja ya majengo ya kihistoria na kivutio maarufu cha watalii katika Visiwa vya Zanzibar, inatarajiwa kufanyiwa ukarabati mkubwa ili kurejeshwa katika hadhi yake ya kimataifa.
Hoteli hiyo iliyopo eneo la Malindi, mjini Unguja, ilijengwa katika miaka ya 1960 kama sehemu ya miradi ya maendeleo baada ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kwa miongo kadhaa, Bwawani ilihudumia wageni maarufu, viongozi wa kitaifa na kimataifa, na kuwa kitovu cha mikutano ya serikali pamoja na sherehe mbalimbali.
Hata hivyo, kutokana na uchakavu na changamoto za kiutendaji, hoteli hiyo ilifungwa kwa miaka kadhaa, hali iliyosababisha malalamiko kutoka kwa wananchi na wadau wa utalii kuhusu kupotea kwa alama muhimu ya historia na utalii wa Zanzibar.
Akizungumza leo Septemba 29 katika kikao chake na wananchi wa Mji Mkongwe kilichofanyika ndani ya Ukumbi wa Hoteli ya Bwawani, Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema hoteli hiyo itafanyiwa uwekezaji mkubwa ili kutoa huduma bora na za kisasa.
“Wapo wapinzani wanaodai kuwa nilikataa mwekezaji aliyetaka kuwekeza dola milioni tatu. Ukweli ni kwamba hoteli hii inahitaji uwekezaji mkubwa zaidi, si huo wa dola milioni tatu pekee,” amesema Dk. Mwinyi.
Kwa mujibu wa Dk. Mwinyi, ukarabati huo utaifanya Bwawani kurejea kuwa alama ya kihistoria na kitovu cha utalii, jambo litakaloongeza hadhi ya Zanzibar kimataifa na kukuza pato la Taifa kupitia sekta ya utalii.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED