Ahukumiwa mwaka mmoja jela kwa wizi wa mita za maji Moshi

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 08:47 AM Mar 27 2025
Mkurugenzi Mtendaji wa MUWSA Mhandisi Kija Limbe.

Mahakama ya mwanzo Wilaya ya Moshi Mjini imemuhukumu kifungo cha mwaka mmoja jela Shafii Kondo (56) mkazi wa mtaa wa Kiusa kwa kosa la kuiba mita za maji za Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA).

Akitoa hukumu hiyo leo Machi 26,2025 Hakimu Aron Mkoi amesema anamuhukumu Shafii kwa kosa la kuiba mita tisa zenye thamani ya shilingi laki tisa na kuisababishia Mamlaka hasara.

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi MUWSA hivi karibuni ilikabiliwa na changamoto ya baadhi ya wananchi wasio waaminifu kuhujumu miundombinu kwa kuiba mita za maji ambazo zimekua zikisababishia Serikali hasara kubwa. 


Akizungumza baada ya hukumu hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa MUWSA Mhandisi Kija Limbe amesema mpaka sasa Mamlaka imepata hasara ya zaidi ya shilingi milioni ishirini na mbili laki tano na sabini na saba elfu (22,577,000/=) ambazo takribai mita 211 zimeibwa kwa kipindi cha kuanzia Oktoba 2024 mpaka mwezi wa pili mwaka huu.

Aidha Mkurugenzi amewataka wananchi hayo ambao sio waaminifu kuacha mara moja kwani kwa sasa Serikali imeweka mbinu mbalimbali za kuwabaini na kuwakamata sambamba na  hatua stahiki kuchukuliwa juu yao.