Asasi za Kiraia zakutana Arusha kujadili Dira ya Taifa 2050

By Cynthia Mwilolezi , Nipashe
Published at 11:47 AM Jun 02 2025
Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society (FCS), Justice Rutenge.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society (FCS), Justice Rutenge.

Asasi za Kiraia (AZAKI) kutoka maeneo mbalimbali nchini zimekutana jijini Arusha kwa mkutano wa siku tano kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo ya Taifa, huku zikiweka msisitizo katika mchango wao kwenye uboreshaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, hususan katika sekta ya elimu na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ufunguzi wa Wiki ya Azaki, Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Society (FCS), Justice Rutenge amesema AZAKI zimekuwa na ushiriki mkubwa katika mchakato wa kutoa maoni kwa ajili ya kuboresha Dira hiyo ya Taifa.

“Tumejikita zaidi katika kuishauri serikali kuhusu namna bora ya kuboresha sekta ya elimu ili iweze kwenda sambamba na maendeleo ya teknolojia duniani. Tunataka elimu yetu iwe ya kimapinduzi kwa kutumia TEHAMA kama chombo cha msingi,” amesema Rutenge.

Aidha, ameeleza kuwa AZAKI zinaendelea kushirikiana na serikali katika kuimarisha uchumi endelevu na kuhakikisha maendeleo ya Taifa yanazingatia ushirikishwaji wa jamii kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya AZAKI, CPA Mercy Silla amesema kuwa wiki hiyo inaakisi miaka saba ya mafanikio tangu kuanzishwa kwake, lengo kuu likiwa ni kuwaunganisha wadau wa sekta hiyo kwa ajili ya kujadili mustakabali wa maendeleo ya Tanzania.

“Kila mwaka tunaweka mada kuu na kuijadili kwa kina. Mwaka huu tumejikita katika mchakato wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku tukisisitiza umuhimu wa AZAKI kujitegemea zaidi badala ya kutegemea wahisani pekee. Tunahitaji mikakati ya kujitegemea kifedha na kimfumo,” amesema.
Picha ya pamoja.

Naye Mkurugenzi Mkazi wa CBM International na Mwenyekiti wa Kamati ya AZAKI, Nesia Mahenge amesema lengo la wiki hiyo ni kujadili changamoto zinazozikumba AZAKI na kutafuta suluhisho la pamoja kwa ajili ya ufanisi wa kazi zao.

Katibu Mkuu wa Baraza la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO), Adamsono Nsimba ameongeza kuwa ni wakati wa AZAKI kupanga mikakati ya kujitegemea ili kujiimarisha bila kutetereka pindi kunapotokea mabadiliko ya kisiasa au kiuchumi duniani.

"Kwa mfano, tulishuhudia jinsi baadhi ya taasisi zilivyoathirika kufuatia mabadiliko ya uongozi nchini Marekani, ambapo baadhi ya misaada ilisitishwa na hivyo kusababisha shughuli nyingi kusimama. Hili ni fundisho kwamba tunapaswa kuwa na vyanzo mbadala vya rasilimali," amesema Nsimba.

Wiki ya Azaki inaendelea kwa midahalo, warsha na mijadala mbalimbali, ikihusisha zaidi ya washiriki 900 kutoka taasisi mbalimbali za kiraia ndani na nje ya nchi.