Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Aida Khenani, amekanusha uvumi unaoenea kwamba anatarajia kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) au chama cha CHAUMMA baada ya kuvunjwa kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza kwa njia ya simu akiwa jijini Dodoma anakohudhuria vikao vya Bunge la Bajeti, Khenani amesema taarifa hizo ni za uzushi na hazina ukweli wowote.
“Mimi bado nipo Chadema. Siwezi kuzungumzia masuala ya CCM wala CHAUMMA. Hata kama nitatoka CHADEMA, kuna utaratibu wa kufuata. Lakini ieleweke kuwa mimi ni mbunge ninayetokana na chama hiki hadi hapo ubunge wangu utakapoisha,” amesisitiza Khenani.
Amesema kwa sasa nguvu yake yote iko ndani ya chama hicho na ataendelea kuheshimu msimamo wa Chadema kuhusu uchaguzi mkuu ujao, hasa iwapo hakutakuwa na mabadiliko ya msingi kwenye sheria za uchaguzi.
“Mungu ndiye anajua kama nitaendelea kuwa mbunge wa jimbo hili katika uchaguzi ujao au la. Kama msimamo wa chama ni kutoshiriki uchaguzi pasipo reform, basi kama mwanachama mwaminifu wa Chadema, nitalazimika kuungana nao,” amesema.
Kauli hiyo imekuja wakati ambapo baadhi ya wanachama wa CHADEMA, hasa kutoka kundi la G-55, wamekuwa wakihama chama hicho na kujiunga na vyama vingine kama ACT Wazalendo na CHAUMMA. Sababu kuu wanayotoa ni kutoridhishwa na msimamo wa chama wao wa juu wa kutoshiriki uchaguzi bila mabadiliko ya sheria za uchaguzi.
Ripoti zisizo rasmi pia zimeeleza kuwa baada ya kuvunjwa kwa Bunge mwishoni mwa mwezi huu, kundi kubwa zaidi la wanasiasa kutoka CHADEMA, wakiwemo baadhi ya wabunge wa viti maalum, huenda wakatangaza rasmi kuhama chama hicho.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED