Waziri wa Maji Jumaa Aweso ameeleza kuwa msukumo wa serikali ndani ya miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imefanikisha kikamilifu kutekeleza ilani ya CCM 2020/25, akieleza kuwa kufikia mwishoni mwa mwaka huu huduma za maji Mijini na Vijijini huenda zikavuka lengo lililokuwa limeweka kwenye Ilani.
Akizungumza Bungeni leo wakati wa kujibu hoja za wabunge zilizoibuliwa wakati wa mjadala wa Hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Waziri Aweso ameeleza kuwa lengo la Ilani lilikuwa ni kuwa na huduma ya maji vijijini kwa asilimia 85 na mijini 95 na kufikia sasa tayari huduma zinapatikana kwa asilimia 83 vijijini na 91 mijini.
Waziri Aweso ameliambia bunge kuwa ipo miradi mingine ya maji 1,000 inayotekelezwa nchi nzima, ambayo kukamilika kwake kutavuka malengo ya ilani, Akimshukuru Rais Samia kwa ongezeko kubwa la bajeti aliloliidhinisha ikiwemo ununuzi wa mitambo ya kuchimba visima na mabwawa ya kuvuna maji ya mvua maeneo mbalimbali ikiwemo Handeni Tanga, Kizengi Tabora na Monduli mkoani Arusha.
"Aina ya Rais kama Samia hapatikani kila mahali, hapatikani kila wakati. Tumempata lazima tumtumie kwa maslahi ya watanzania na hapa ninachotaka kusema rais ni suluhu ya matatizo ya watanzania," amesema Aweso.
Pia Aweso aliishukuru Wizara ya fedha kwa ushirikiano wao mzuri kwenye sekta ya maji, akisema kwasasa wizara yake haina kisingizio chochote, na kwamba kupitia Wakala wa Huduma za Maji Vijijini (Ruwasa), tayari vijiji takribani 10, 000 vimeshaunganishiwa huduma ya maji.
"Vijiji vilivyosalia ni 2,000 pekee lakini lengo la serikali ya awamu ya sita ni kuhakikisha kuwa vijiji vyote 12,318 vinapata huduma ya maji kufikia mwishoni mwa mwaka huu," amesema Aweso.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED