Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) John Mnyika amesema ni jambo la kushangaza na kusikitisha kuona wananchi wakizuiwa kuingia mahakamani wakati maafisa wa polisi wamejazana ndani ya ukumbi wa Mahakama.
Amesema iwapo kesi hiyo ni ya haki na inasikilizwa kwa uwazi, haoni sababu ya wananchi, waandishi wa habari na wadau wa haki kuzuiwa kushiriki mchakato huo muhimu.
“Kwa sababu hiyo, tumeamua kutoka nje ya Mahakama kama njia ya kuonesha msimamo wetu. Tunatuma ujumbe wa wazi kwamba kama Mahakama imeamua kuendesha shughuli zake kwa usiri na bila uwazi, basi waendelee peke yao – lakini si kwa jina la haki,” amesema.
Katibu Mkuu huyo alibainisha kuwa wamezungumza na uongozi wa Mahakama ambao umeahidi kuwasiliana na askari waliopo nje ili kuhakikisha wananchi wanaruhusiwa kuingia kushuhudia mwenendo wa kesi kama inavyotakiwa kisheria.
Aidha, alisisitiza kuwa CHADEMA haitakubali kuingia tena ndani ya Mahakama hadi pale haki itakapokuwa ikitendeka kwa uwazi na wananchi wote, wakiwemo waliotoka mbali kwa gharama kubwa na matumaini ya kupata haki, watakapopewa nafasi yao ya kikatiba kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kusikiliza kesi.
“Haki haifanywi kwa siri. Haki ni ya watu wote. Na tutasimama hadi haki itendeke,” amehitimisha.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED