JESHI la Polisi mkoani hapa limetaja chanzo cha ajali ya basi lililojeruhi wabunge, watumishi wa Bunge na watu wengine jumla yao 23 kuwa ni uzembe wa dereva kushindwa kuchukua tahadhari alipotaka kulipita gari lingine barabarani.
Kutokana na uzembe huo, Jeshi la Polisi linamshikilia kwa mahojiano dereva huyo, Bahati Saidi, kutoka Kampuni ya Shabiby, ambaye pia ni miongoni mwa majeruhi wanaoendelea na matibabu.
Jumatano ya wiki hii, Rais Samia baada ya kutokea ajali iliyohusisha magari matatu na kuua watu saba na kujeruhi tisa, alilielekeza Jeshi la Polisi kuhakikisha madereva wanaongeza umakini na kuzingatia sheria za barabarani, hasa kipindi hiki cha mwisho wa mwaka ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika.
Pia aliagiza uhuishaji na uwekaji wa alama za barabarani kwenye maeneo hatarishi na kuzingatia umbali na maeneo sahihi ya uwekaji wa vituo vya ukaguzi ili vionekane kwa urahisi zaidi.
Akizungumzia jana ajali hiyo ya wabunge, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) George Katabazi, alisema ilitokea saa 2:00 asubuhi katika barabara kuu ya Dodoma- Morogoro, eneo la Mbande, wilayani Kongwa.
Kamanda Katabazi alisema kati ya waliojeruhiwa, wabunge ni 17, maofisa wa Bunge wawili, askari wawili, dereva na kondakta.
Kamanda Katabazi alisema wabunge hao walikuwa wakisafiri kwenda Mombasa, Kenya kushiriki Mashindano ya 14 ya Mabunge ya Afrika Mashariki.
Alisema basi hilo limegongana uso kwa uso lakini dereva wa lori alijaribu kuchukua tahadhari ili wasigongane na alipanua kidogo njia ili kulipisha gari lililokuwa likipita lakini basi likagonga tela la lori.
Kwa mujibu wa SACP Katabazi, majeruhi hao wamelazwa katika Hospitali ya Kanda za Rufani ya Benjamin Mkapa, Kongwa, Chamwino na wengine wamepelekwa Hospitali ya Rufani ya Mkoa Dodoma na wanaendelea na matibabu vizuri na hakuna kifo chochote kilichotokea.
“Eneo hilo alilotaka kulipita gari hilo haliruhusiwi kupita gari lililo mbele.Kuna mistari ya katazo ya kutolipita gari lililo mbele yake lakini dereva hakuzingatia hilo na matokeo yake amesababisha ajali hiyo.
“Kama mnavyoona alitoka nje zaidi ya barabara baada kugonga tela hilo na kushindwa kulimudu gari na kutoka nje ya barabara zaidi ya mita 10 hadi 15,” alisema.
Kamanda Katabazi alisema wanamshikilia dereva huyo kwa mahojiano zaidi na hatua nyingine za kisheria zitazingatiwa.
“Ajali hii imesababisha majeruhi na uharibifu wa magari. Kwa hiyo marereva wakizingatia sheria za usalama barabarani ajali zitaepukika. Ni muhimu wazingatie sheria kwa kuwa kilichotokea ni uzembe na kutozingatia sheria husika,”alisema.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano katika Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH), Jeremiah Mwakyoma, alithibitisha kupokewa kwa baadhi ya majeruhi wa ajali hiyo na kwamba wanaendelea na matibabu huku hali zao zikiendelea vizuri.
Akizungumza mara baada ya kuwajulia hali majeruhi hao, Waziri wa afya, Jenister Mhagama, alisema wamepokea majeruhi 23 na wote wanaendelea vizuri.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED