DC Tanga akoshwa na huduma za PSSSF

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:18 AM Jun 02 2025
DC Kolimba akielezwa huduma zitolewazo na PSSSF maonesho ya biashara na utalii Tanga.
Picha:Mpigapicha Wetu
DC Kolimba akielezwa huduma zitolewazo na PSSSF maonesho ya biashara na utalii Tanga.

Mkuu wa Wilaya ya Tanga Dadi Kolimba ameupongeza Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa kuendana na kasi ya teknolojia kutoa huduma kidigitali.

Pongezi hizo zimetolewa katika Maonesho ya 12 ya Biashara na Utalii yanayoendelea katika Viwanja vya Mwahako alipotembelea banda la maonesho la Mfuko.

Awali Afisa Mfawidhi PSSSF Tanga,Suleiman Majingo, alisema, miongoni mwa maboresho ya Mfuko katika serikali ya awamu ya nne ni kwenye eneo la malipo ya mafao ya wastaafuu waliokua wakipokea kima cha chini.

 “Kuanzia Januari mwaka huu kima cha chini cha malipo ya pensheni kimepanda kutoka Sh 100,000 kwa mwezi hadi Sh 150,000 kwa mwezi,” alifafanua. 

Aidha, alisema maboresho mengine ni mstaafu akifariki wategemezi wake watapewa Sh 500,000 za msaada wa maziko na malipo ya pensheni ya mstaafu kwa miezi 36. 

Hali kadhalika PSSSF imefanya maboresho mengine katika eneo la utoaji wa huduma, ambapo Mfuko umeendelea kuwa kinara katika kuwahudumia wanachama kupitia TEHAMA.

“Kupitia PSSSF Kidijitali, mwanachama kwa kutumia simu janja au kompyuta, anaweza kuangalia michango yake, mafao, kuwasilisha madai mbalimbali, kuuliza maswali na kupatiwa majibu, pia wastaafu wanaweza kujihakiki kupitia simu janja, hii imeondoa usumbufu na kupunguza gharama kwa wanachama wetu na mfuko pia,” aliongeza.