DCEA yaonya wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 08:59 PM Jul 05 2025
Kamishina Jenerali wa mamlaka hiyo, Aretas Lyimo akizungumza kwenye maonesho hayo
Picha: Elizabeth Zaya
Kamishina Jenerali wa mamlaka hiyo, Aretas Lyimo akizungumza kwenye maonesho hayo

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)imewaonya wale wanaoendela kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Imesema hakuna anayejihususha na biashara hiyo haramu atakayebaki salama kwa kuwa kazi ya kuwabaini wote wanaojihusisha na biashara hiyo inafanyika usiku na mchana.

Akizungumza katika Maonesho ya Biashara ya 49 ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF) maarufu Sabasaba, Kamishina Jenerali wa mamlaka hiyo, Aretas Lyimo amesisitiza watakaokaidi maelekezo ya serikali hatua za kisheria zitachukua mkondo wake na wataendelea  kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Pia amesema wale wote watakaoendelea kutangaza, kusifia au kuhamasisha matumizi ya dawa za kulevya iwe kwa mavazi, nyimbo au namna yoyote ile hatua za kisheria zikachukuliwa dhidi yao.

Amesema na ndani ya sheria kuna vifungu vya sheria hususani kifungu namba 24 kinachoeleza kwamba yeyote yule anayehamasisha matumizi dawa za kulevya anachukuliwa hatua kama wahalifu wengine.

Amewaomba watanzania waachane na biashara ya matumizi ya dawa za kulevya, uzalishaaji na usambazaji wa dawa hizo na kuwaomba wazazi wahakikishe wanalinda watoto wao wasijiingize kwenye matumizi au biashara hiyo.

Kuhusu hali ya dawa za kulevya nchini, Kamishna Jenerali Lyimo amesema kwa sasa hali inaendelea kuwa nzuri na inaendelea kuimarika kutokana na operesheni mbalimbali zinazoendelea kufanywa na mamlaka hiyo kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.

Akieleza ushiriki wa mamlaka hiyo katika maonesho hayo amesema  lengo ni kuwapa wananchi elimu ili wajue aina ya dawa za kulevya pamoja na sheria zinazokataza biashara hiyo.

“Na sasa hivi tuko katika operesheni maalum ya kuhakikisha tunatoa elimu maalum kwa wanafunzi wa elimu ya msingi sekondari na vyuo lakini tunafanya operesheni maalum ya kukamata wale wote ambao bado wanaendelea kujihusisha na biashara ya usambazaji na uzalishaji wa dawa za kulevya.

“Lengo ni kuhakikisha kwamba ndani ya kipindi kifupi tunamaliza kabisa tatizo la dawa za kulevya nchini lakini wananchi wanapata uelewa wa kutosha kuhusu dawa za kulevya."