Klabu ya Yanga iko mbioni kukamilisha usajili wa straika, Celestin Ecua, raia wa Ivory Coast, ikizipiku Simba na Azam FC ambazo nazo zilikuwa zikimuwania nyota huyo.
Taarifa zilizopatikana jana kutoka vyanzo mbalimbali vya ndani ya klabu hiyo na nje ya nchi, zinasema makubaliano baina ya pande zote mbili yameafikiwa, kilichobaki ni kusaini mkataba kwa mchezaji hiyo anayekipiga kwenye klabu ya Zoman ya nchini humo.
Kabla ya kujiunga na timu hiyo, Ecua, alikuwa akiichezea, Asec Mimosas.
Akiwa kwenye kikosi cha Zoman msimu uliopita, alipachika mabao 15 na 'asisti' 12, na kuisaidia timu hiyo kumaliza ligi kwenye nafasi ya tisa katika msimamo ikivuna pointi 37.
Nyota huyo anakuwa mchezaji wa pili kutajwa kwenye orodha ya wachezaji watakaovaa jezi za njano na kijani msimu ujao kutoka Ivory Coast, baada ya kiungo mchezeshaji, Mohamed Doumbia (26), aliyekuwa akiichezea FC Slovan Liberec ya Jamhuri ya Czech.
Yanga pia imetajwa pia kuwinda saini za winga, Miguel Vieira, maarufu kama Gilberto wa Orlando Pirates, raia wa Angola, anayecheza kwa mkopo kwenye klabu ya Petro de Luanda ya Angola, beki wa kulia wa TP Mazembe, Ibrahim Keita, raia wa Mauritania, ingawa tayari imepata upinzani kutoka kwa Esperance ya Tunisia ambayo nayo imejitosa kutaka saini yake na kiungo mkabaji, Daba Benoit Diakite, raia wa Mali,
Majuzi, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Klabu ya Yanga, Alex Ngai, alibainisha kwa sasa wanafanya usajili mkubwa kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, baada ya kuliteka na kulitawala soka la hapa nchini.
"Humu ndani ya nchi tumeshamaliza kila kitu, hatudaiwi, kuanzia msimu ujao mawazo, nguvu na akili zetu tunataka tufanye vizuri kwenye michuano ya kimataifa, Ligi ya Mabingwa Afrika.
Pamoja na yote msimu huu hatukufanya vizuri kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa, tulitolewa kwenye makundi, kwa hiyo usajili kama kawaida ni lazima ufanyike, tunaangalia sehemu ambazo zina mapungufu tuzirekebishe.
Pia alisema usajili kwa sasa unaendelea, nadhani tutaingiza wachezaji wazuri sana kwenye maingizo mapya, nawaahidi wanachama na mashabiki wa Yanga kuwa tunafanya usajili ulio bora kwa ajili ya mechi za kimataifa msimu ujao," alisema Ngai.
Wakati hayo yakiendelea klabu ya Yanga imesema kikosi kitakachoundwa msimu ujao, kitakuwa kimetengenezwa na ripoti za makocha watatu ambao wote wameondoka na kuacha mafaili yanayoonyesha mapungufu na jinsi ya kukiimarisha kikosi chao.
Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe, amesema makocha walioondoka na kuacha ripoti zao ambazo zote zinafanyiwa kazi na uongozi ni Miguel Gamondi, Saed Ramovic na Miloud Hamdi.
Alisema kutokana na hali hiyo, anatengemea kikosi cha msimu ujao kitakuwa moto wa kuotea mbali, kwani kitakuwa kimefanyiwa kazi kutokana na mwongozo na maono ya makocha wote hao walioifundisha timu hiyo kwa vipindi tofauti.
"Hivi ninavyokwambia tayari tunaye kocha mpya ambaye tutamtangaza hivi karibuni. Atakuja kuongezea tu pale ambapo makocha watatu wamepafikisha.”
“Wote wameacha ripoti kuanzia Gamondi, Ramovic na Miloud, kila mmoja kwa wakati wake ameanisha wapi ambapo tupo sawa, tupo imara, sehemu gani ambapo kuna udhaifu, na nini kifanyike ili kikosi kiwe imara msimu ujao," alisema Kamwe.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED