Watanzania Sweden waadhimisha siku ya lugha ya kiswahili duniani

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 02:49 PM Jul 06 2025
news
Picha Mpigapicha
Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mobhare Matinyingumza katika sherehe za siku ya Kiswahili Duniani

UBALOZI wa Tanzania nchini Sweden kwa kishirikiana na jumuiya za Watanzania waishio nchini humo, umeandaa na kufanikisha sherehe za maadhimisho makubwa ya Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika Jualai 5, mwaka huu , jijini Stockholm.

Maadhimisho haya hufanyika duniani julai 7 ya kila mwaka kuanzia mwaka 2022 kufuatia azimio lililopitishwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO).

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Balozi wa Tanzania nchini humo, Mobhare Matinyi, amesema Serikali imeazimia kukieneza na kukienzi Kiswahili duniani kote huku akielezea namna kilivyosambaa na kuongeza kuwa kwa ushawishi wa Tanzania, Kiswahili sasa ni lugha ya kikazi Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Waziri wa zamani wa Usawa na Jinsia nchini Sweden, Nyamko Sabuni, ambaye alielezea namna kiswahili kinavyoziunganisha nchi hizi akibainisha hata anapokuwa nchini Kenya kibiashara hutumia pia lugha hiyo.

Sherehe hizo zilifana kwa wingi wa vyakula na vitu mbalimbali vinavyoitangaza Tanzania na utamaduni wa Mswahili kama viungo, maonesho ya mitindo ya mavazi, sanaa za mapambo, ngoma, nyimbo, mashairi na hadithi za watoto.

Shughuli hiyo iliwakutanisha zaidi ya watu 500 ambao mbali ya Watanzania wengine walikuwa ni raia au wenye asili za nchi za Afrika Mashariki na Kati, Waswidi marafiki wa Tanzania na Mabalozi na wawakilishi wa nchi za Botswana, China, Eritrea, India, Japan, Kenya, Misri, Nigeria, Rwanda na Zimbabwe. 

Wadhamini walioshirikiana na Ubalozi ni benki mbili za nchini, NMB na CRDB; Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Kenzan Travel, Green Tours Tanzania na Monty's Glow.