Sheikh Ponda atoa kauli hali ya kisiasa nchini

By Imani Nathaniel , Nipashe
Published at 01:59 PM Jul 06 2025
news
Picha Imani Nathaniel
Kada wa chama cha ACT-Wazalendo, Sheikh Issa Ponda

KADA wa chama cha ACT-Wazalendo, Sheikh Issa Ponda, ametoa wito kwa wananchi kuchukua hatua dhidi ya kile alichokitaja kuwa ni mfumo wa kisiasa usio ridhisha unaodhoofisha misingi ya demokrasia nchini.

Akizungumza leo katika mkutano mkuu wa jimbo la Temeke, Sheikh Ponda amesema tangu uchaguzi wa mwaka 2020 kumekuwa na kilio cha mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi, lakini hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa hadi sasa.

“Tume ya uchaguzi haijafanyiwa marekebisho ya kisheria ili iwe huru na isiyoegemea upande wowote. Sheria kandamizi dhidi ya vyama vya siasa bado zipo na mfumo wa uandikishaji wa wapiga kura hauhakiishi usawa,” amesema.

Sheikh Ponda amesisitiza kuwa Tanzania ni ya Watanzania wote na haipaswi kuendelea kuwa mali ya wachache wanaotumia hila, vitisho na mizengwe kuwa katika madaraka.

Aidha, katika kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba, Sheikh Ponda ametoa wito kwa wananchi kuchukua hatua muhimu ikiwemo kujitokeza kwa wingi kupiga kura, kulinda kura kwa umoja na ujasiri, kuhakikisha mshindi halali anatangazwa.

Waachama wa ACT-Wazalendo
Naibu Katibu Mkuu wa Vijana wa ACT-Wazalendo Ruqayya Nassir amesema wanaenda kwenye uchaguzi ambao wanatakiwa kupambana na kushikamana kama chama ili waweze kupata ushindi.

“Umoja wetu ndio utafanya chama chetu kiweze kupata viongozi wengi katika uchaguzi wa Oktoba, mwaka huu, hivyo hatupaswi kuwa waoga katika kupambania maslahi ya chama chetu,” amesema Nassir. 

Naye, mjumbe wa halmashauri kuu ya chama hicho, Joram Bashange, amesema kususia uchaguzi mda mwingine sio busara kwakuwa inaweza kupoteza haki za wanachama huku akitolea mfano wa nchi ya Bangladesh iliyosusia uchaguzi na kukipa chama tawala nguvu mara dufu.

“Chama kisiposhiriki uchaguzi kinakuwa kimejiuwaa na kukipa nafasi ya kuendelea kuongoza chama kinachopambana nacho,” amesema.