Vijana waitwa kuchangamkia fursa mikopo

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 05:41 PM Jul 06 2025
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete (katikati)
Picha: Mpigapicha Wetu
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete (katikati)

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete ametoa wito kwa vijana kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo katika Ofisi ya Waziri Mkuu, ikiwamo mikopo ya Vijana kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Mifuko ya Uwezeshaji Kiuchumi.

Ridhiwani ametoa wito huo, alipotembelea Banda Jumuishi la Ofisi ya Waziri Mkuu Pamoja na Taasisi zake katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba Jijini Dar es Salaam.

Aidha amesema kuwa lengo la Ofisi hiyo katika maonesho hayo ni kuendelea kutoa elimu   zaidi kwa vijana kuhusu fursa za kiuchumi zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kuhakikisha vijana wanajiinua kiuchumi.

Amesema kuna fursa nyingi zinatolewa na serikali kupitia mikopo inayolenga makundi maalum,mikopo kutoka mifuko ya uwezeshaji kiuchumi hivyo vijana wanapaswa kuchangamkia fursa hizo.

"Naomba vijana tuchangamkie fursa za mikopo zinazotolewa na mfuko wa maendeleo ya vijana na mifuko ya uwezeshaji kiuchumi,tusibaki nyuma hususani vijana wa kiume," amesema Kikwete.

Amesema kwa upande wa vijana wa kike takwimu zinaonyesha wako vizuri kwenye kuchangamkia fursa hivyo na nyie vijana wa kiume changamkieni fursa ili kujiinua kiuchumi katika maeneo mbalimbali.

Halikadhalika Ridhiwani amewaagiza maafisa Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake kuendelea kutoa elimu na kuhakikisha inakuwa kipaumbele kikubwa kwa wananchi ili wapate uwelewa nini serikali yao inafanya kwa upande wa vijana.