Bodi Maktaba kuongeza nia usomaji vitabu kwa jamii

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 05:31 PM Jul 06 2025
Mkurugenzi wa Uendeshaji Maktaba kutoka TLSB, Dk. Rehema Ndumbaro (katikati)
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi wa Uendeshaji Maktaba kutoka TLSB, Dk. Rehema Ndumbaro (katikati)

ILI juhudi za kukuza utamaduni wa kusoma miongoni mwa Watanzania, Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB) imeanza ujenzi wa maktaba 15 za kijamii katika maeneo mbalimbali nchini.

Maktaba hizo, zinatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba 2025, ni sehemu ya mkakati wa serikali kuhakikisha maarifa yanawafikia wananchi moja kwa moja, hususan vijana na wakazi wa vijijini ambako huduma za maktaba zimekuwa adimu kwa muda mrefu.

Hatua hiyo inakuja kufuatia uhalisia kwamba Watanzania wengi bado hawajapata mwamko wa kusoma vitabu kwa hiari hali ambayo inakwamisha maendeleo ya kijamii, kielimu na kiuchumi.

Akizungumza katika kongamano la waandishi lililofanyika jana jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuhamasisha uandishi unaoleta mabadiliko katika jamii, Mkurugenzi wa Uendeshaji Maktaba kutoka TLSB, Dk. Rehema Ndumbaro, amesema maktaba hizo zinalenga kuongeza ari ya usomaji wa vitabu kwa wananchi katika maeneo yao.

“Mpaka sasa huduma za maktaba zinapatikana katika mikoa 22 na wilaya 19 na lengo letu ni kuhakikisha kila mkoa nchini unakuwa na maktaba ifikapo mwaka wa fedha 2025/2026,” amesema Dk. Ndumbaro.

Ameongeza kuwa, sambamba na uboreshaji wa miundombinu, TLSB imewekeza katika ununuzi wa vitabu kutoka kwa waandishi wa ndani. “Kwa mwaka huu pekee, tumenunua zaidi ya vitabu 19,000 kutoka kwa waandishi wa Kitanzania,” amebainisha.

Amewahimiza waandishi na watunzi wa vitabu kuzingatia uzalendo na mahitaji ya wananchi, wakitazama Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2030 na ile ya 2050, ili kusaidia juhudi za serikali katika kuelimisha jamii.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ubunifu na Uandaaji wa Vifaa vya Kielimu kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Fixon Mtelesi, amesema taasisi hiyo inaendelea kusimamia miongozo mbalimbali ya elimu kwa ajili ya kuzalisha vitabu vinavyolenga kuwasaidia wanafunzi na jamii kwa ujumla.

Amebainisha kuwa TET pia imebeba jukumu la kuwaelimisha waandishi na watunzi wa vitabu namna ya kuandika maudhui yanayohitajika, ili kuchangia ukuaji wa sekta ya elimu na kuongeza maarifa kwa wasomaji.

“Bado kuna changamoto ya usomaji wa vitabu nchini. Watanzania wengi hawapendi kusoma, hivyo ni vyema watunzi na waandishi wakaandika vitabu vyenye maudhui yanayowagusa moja kwa moja,” amesema Mtelesi.

Mwenyekiti wa Umoja wa Waandishi wa Vitabu Tanzania, Anna Mbise, amesema moja ya changamoto kubwa inayowakabili ni tabia ya wasomaji kupendelea maudhui yanayotoa majibu ya moja kwa moja badala ya yale yanayowapa nafasi ya kutafakari kabla ya kufanya maamuzi.

Naye mwandishi wa vitabu, Johnson William, amesema TET ina wajibu wa kusaidia kukuza kundi la waandishi nchini kwa kulenga maandalizi ya maudhui yenye soko ndani na nje ya nchi.

Aidha, amehimiza matumizi ya teknolojia mbadala kama njia ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. “Watunzi na waandishi wanapaswa kupunguza matumizi ya karatasi na badala yake kutumia teknolojia mbalimbali, zikiwemo mbinu za akili bandia, kuchapisha vitabu vya kidijitali,” amesisitiza.

Kongamano hilo limeandaliwa na serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, wakiwemo Taasisi ya Tanzania Young Writers Initiative (TAYOWI), ambayo inawahamasisha vijana kushiriki katika uandishi wa vitabu ili kuelimisha na kuibadilisha jamii.