Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imetoa rai kwa wazabuni kutumia Moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko katika mfumo wa NeST ili kuokoa muda na gharama zisizo na ulazima.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Mtendaji wa PPAA, James Sando alipoongea na waandishi wa Habari katika banda la Mamlaka hiyo kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.
Sando amewasihi wazabuni kuitika wito wa Serikali wa kutumia mfumo wa NeST ambapo ndani ya mfumo huo kuna moduli ya kuwasilisha malalamiko na rufaa, hivyo watumie fursa hiyo kuwasilisha malalamiko na rufaa zao.
“Moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko katika mfumo wa NeST ni suluhisho kwa wazabuni katika kuwasilisha rufaa pindi wanapokuwa hawajaridhishwa na mchakato wa ununuzi wa umma katika zabuni walizoshiriki,” amesema Sando
Sando aliongeza kuwa baada ya matumizi ya moduli kuanza rasmi mwezi Februari 2025 mzabuni halazimiki kufika ofisi za Mamlaka ya Rufani kuwasilisha rufaa, badala yake atamie moduli kuwasilisha rufaa husika kupitia mfumno wa NeST.
Aidha, Sando ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2025/26 PPAA inatarajia kuanza kusikiliza mashauri kwa njia ya mtandao ili kurahisisha zaidi usikilizaji wa rufaa pale itakapoonekana kuna ulazima wa kufanya hivyo.
Pamoja na mambo mengine,Sando amesema moduli ina faida nyingi hususan kuokoa muda na grahama, imerahisisha upatikanaji wa nyaraka, kutunza kumbukumbu pamoja na kuongeza uwazi na uwajibikaji.
Katika kuhakikisha kuwa matumizi ya moduli yanawafikia wazabuni wengi kwa wakati uliokusudiwa, PPAA imeshatoa mafunzo ya namna ya kuwasilisha malalamiko na rufaa kwa njia ya kieletroniki katika kanda mbalimbali ambapo mpaka sasa Kanda ya Pwani, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Kati zimepatiwa mafunzo.
Aidha, katika mafunzo hayo PPAA imefanikiwa kutoa elimu kwa wazabuni 873 na wakuu wa idara/vitengo vya ununuzi na sheria wapatao 1,588 kutoka katika taasisi nunuzi 500.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED