Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umesema upo umuhimu kwa jamii kushiriki upandaji miti na kuunga mkono juhudi za serikari kushiriki katika usimamizi endelevu wa misitu kama nguzo ya kulinda vyanzo vya maji, kuhifadhi bioanuwai, kuhimili mabadiliko ya tabianchi na kukuza uchumi wa taifa.
Akizungumza leo, muda mfupi kabla ya ufunguzi wa siku ya Mazingira katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Meneja wa Sehemu ya Baiolojia ya Mbegu za Miti TFS, Fandey Mashimba, amesema Tanzania inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha upandaji miti unakuwa endelevu na wenye tija.
Kwa mujibu wa Mashimba, Tanzania inakadiriwa kuwa na hekta milioni 48.1 za misitu, sawa na asilimia 55 ya eneo la ardhi la Tanzania Bara, ambapo zaidi ya nusu ya misitu hiyo ipo chini ya usimamizi wa serikali kuu, serikali za vijiji na mamlaka za mitaa.
“Kwa mwaka tunakadiria upotevu wa hekta zaidi ya 469,000 kutokana na kilimo cha kuhama hama, uvunaji haramu, matumizi ya kuni na mkaa yasio zingatia utaratibu wa kisheria.
"Upandaji miti wa kimkakati ndiyo suluhisho, hivyo ni lazima tupande miti kwa wingi na miti sahihi kulingana na ikolojia zake” amesema Mashimba.
Mashimba amewataka wananchi, sekta binafsi na washirika wa kimataifa kushirikiana na TFS na serikari kwa ujumla katika juhudi za uwekezaji katika miradi ya upandaji miti.
Pia, amewataka kuitunza ili hatimae miti hiyo isaidiane na misitu katika kulinda vyanzo vya maji, kukabiliana na upungufu wa rasilimali za misitu na kuboresha mifumo ya ikolojia.
Amesisitiza wadau wa mazingira, matumizi ya mbegu bora za miti ambazo vyanzo vyake ni misitu ya kupanda na asili.
Kadhalika, amesema kuwa, TFS inahitaji miche milioni 440 kila mwaka ili kufikia lengo la kurejesha ardhi iliyoharibiwa na kutimiza ahadi za kitaifa na kimataifa kama AFR100 ambapo TFS ni mratibu wa Kitaifa na kwamba bila ushiriki wa wadau wengine siyo rahisi kufanikisha hilo.
Mashimba amesema mbali na kuhifadhi maji na bioanuwai, misitu inatoa ajira na kipato kupitia biashara ya mazao ya misitu, ufugaji nyuki na utalii wa ikolojia.
Amesema, miradi ya kaboni ni fursa muhimu ya mapato na kupunguza gesi joto, huku akisisitiza haja ya kutoa elimu kwa jamii ili mikataba inayoingiwa ifuate miongozo ya kitaifa na kimataifa kwa maslahi ya nchi na jamii zinazozunguka misitu hiyo.
Katika kampeni za upandaji miti, Mashimba ametaja changamoto mbalimbali ambazo hujitokeza ikiwa ni pamoja na kufa kwa miche kutokana na uangalizi hafifu hasa kwenye maeneo ya vijijini.
Nyingine ni ushiriki mdogo wa sekta binafsi, kutokuwapo na mipango ya matumizi bora ya ardhi pamoja na migogoro ya ardhi na kwamba TFS inaendelea kushirikisha serikali, asasi za kiraia na taasisi za utafiti kama SUA na TAFORI ili kuimarisha juhudi za pamoja.
Mashimba amesema ushirikiano wa wadau wote ni muhimu ili Tanzania ibaki kuwa ya kijani kwa vizazi vijavyo.
“Misitu ni uhai wa sekta nyingine kama vyanzo vya maji na uchumi wa misitu, upandaji na utunzaji wa miti ni msingi wa uhifadhi wa mazingira na unachangia kufikia malengo ya kitaifa na kimataifa,” amesema Mashimba.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED