ACT yataka fedha za uchaguzi zisitumike kupora demokrasia

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 11:57 AM Jul 06 2025
news
Picha Halfani Chusi
Kiongozi wa wa Chama Cha ACT Wazalendo Dorothy Semu

KIONGOZI wa Chama Cha ACT Wazalendo Dorothy Semu ameitaka serikali kuhakikisha Sh. Trilion moja iliyotengwa kwaajili ya uchaguzi inatumika kuimarisha demokrasia na sio kupoka uhuru wa watu kuchagua kiongozi wanayemtaka.

Dorothy ameyasema hayo juzi Bariadi mkoani Simiyu katika mwendelezo wa ziara yao ya 'operesheni majimaji' yenye nia ya kuwahamasisha wananchi kulinda kura zao.

Amesema wanakwenda kushiriki uchaguzi kulinda kura pamoja na kuwawezesha wananchi kuleta mabadiliko kwa kuchagua viongozi wanao wataka.

Pia amesema wanakwenda kwenye uchaguzi ili kupata nafasi ya kuwasemea vijana wanao tafuta ajira, wastaafu wanaokumbana na vikokotoo, kuhakikisha wanalinda masilahi ya Mtanzania aliyeko mahali popote katika nchi yetu.

"Serikali imetenga bajeti ya sh Trilion moja kwaajili ya uchaguzi...tunaikumbusha fedha hizo zinatakiwa zitumike kuboresha na kulinda demokrasia hususani haki ya watanzania kuchagua viongozi wao.

"Tunaiomba serikali fedha hizo zisitumike kupora demokrasia serikali ihakikishe Tume Huru ya Uchaguzi INEC, inafanya mchakato huru wa kuwapatia makamishna wapya ambao sio makada wa CCM. Tunataka tume itakayo simamia uchaguzi kwa haki na haitapendelea chama chochote" amesema Dorothy 

Amesema watanzania wamechoshwa na mchakato wa uchaguzi kwa makosa madogo yanayowafanya wagombea wa vyama pinzani waenguliwe na kwamba wanataka serikali ihakikishe mawakala wa vyama vya upinzani wanaapishwa kwa wakati na wanapewe fursa sawa.

Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa Chama hicho bara, Abduli Nondo amesema uchaguzi ndio fursa muhimu ya wananchi kuonyesha mamlaka yao kwa kuchagua viongozi wanao wataka.

Amesema tangu nchi imepata uhuru tumepata uhuru tumetawaliwa na chama kimoja CCM na kwamba kuwapo kwao madarakani kwa muda mrefu wanawaona wananchi ni watumwa na wao ni mabosi.

"Tunakwenda kuchagua wabunge na madiwani kwa sababu tunataka uwakilishi wa mtu atakaye tusemea kupata huduma za kijamii kama maji barabara na umeme.

"Mnapokwenda kuchagua Mbunge mnachagua mwakilishi wa kwenda kuhakikisha anaisimamia serikali kwa manufaa ya wananchi.

"Leo hii bunge limepoteza thamni na hadhi kwa sababu uchaguzi umekuwa wa...Polisi wamechagua upande kwa kutetea CCM na kushiriki kwenye wizi kipindi cha uchaguzi," amesema Nondo 

Amesema Simiyu imebalikiwa dhahabu lakini wananchi hawanufaiki nazo na kwamba zonanufaisha watu wachache na hivyo hali hiyo hakuna usawa katika ugawaji wa laslimari.

"Ndio maana kwenye shamba lako kukigundulika na dhahabu unakuja kufukizwa na serikali unaambiwa hili sio eneo lako wakati ilitakiwa na wewe unufaike na ile dhahabu," amesema Nondo