Simba yaivamia JKT Tanzania

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:19 AM Jul 06 2025
news
Picha Mtandao
Msemaji wa Klabu ya Simba Ahmed Ally.

Klabu ya Simba imetajwa kuwa mbioni kuinasa saini ya beki wa kushoto wa JKT Tanzania, Karim Mfaume Bakari, ili kumsaidia Mohamed Hussein 'Tshabalala' msimu ujao wa mashindano.

Uhitaji wa beki huyo unaendeleza mpango wa klabu hiyo kutaka kuchukua wachezaji kadhaa wa JKT Tanzania, wakiwemo beki wa kati, Wilson Nangu pamoja na golikipa, Yacoub Suleiman.

Habari zinasema mbali na kutaka kuzoa wachezaji wa maafande hao, Simba pia imetajwa iko mbioni kumalizana na kiungo mkabaji wa Fountain Gate, Abdallah Kulandana.

Taarifa zinasema klabu ya Simba imeanza usajili kwa wachezaji wa ndani ambao tayari wameonekana kuwa na uwezo, pamoja na wale ambao Kocha Mkuu, Fadlu Davids amewaorodhesha.

Kulandana ni mmoja wa wachezaji ambao kocha Fadlu, aliwaambia mabosi wa Simba kuwa anahitaji saini yake baada ya kumuona katika michezo yote miwili ambayo Simba ilicheza dhidi ya Fountain Gate kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

"Tunataka kusajili kwanza wachezaji wa kizawa tumalize ili tuanze kutoka nje ya nchi kusajili wageni ingawa tayari tumeshaanza mazungumzo nao.”

“Hatutaki kijirudie kile cha msimu uliopita, mnaanza kusajili kumbe kuna watu kazi yao ni kuchafua tu, yalijitokeza na Lameck Lawi, Velentino Mashaka, Awesu Awesu, kila tunapogusa, tayari kuna maadui wanakwenda kuweka mkono ili mradi tu tupate ugumu na tuonekane hatuwezi kusajili," kilisema chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo.

Usajili wa Simba umenza baada ya kumalizika kwa kikao cha Bodi ya Wakurugenzi chini ya Mwenyekiti, Mohamed Dewji na Makamu Mwenyekiti, Murtaza Mangungu, ilipokutana na Bodi ya Washauri hivi karibuni.

Kwa mujibu wa Meneja Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally, klabu imeweka mikakati ya siri kuelekea kwenye kipindi cha usajili.

"Kilichomriwa ni namna gani tunavamia soko la usajili, tunaboresha vipi kikosi chetu ili tupambane zaidi. Tumefanikiwa eneo la kujenga timu, lakini tumefeli kukosa makombe yote, kwa hiyo mipango iliyopo ni kuhakikisha msimu ujao tunaongeza ubora wa kikosi ili kutwaa mataji," alisema Ahmed.

Simba imekosa mataji yote iliyokuwa ikipigania msimu huu, ikianzia na Ngao ya Jamii, Kombe la Shirikisho Afrika, Ligi Kuu, pamoja na Kombe la FA.