Klabu ya Azam FC, imemtangaza, Florent Ibenge, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kuwa Kocha Mkuu wa kikosi chao, huku akiweka mikakati ya kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu na mashindano ya kimataifa msimu ujao.
Azam imemtangaza kocha huyo jana jioni kwenye hoteli moja katikati ya jiji kuchukua nafasi ya Rachid Taoussi na atakuwa na jukumu la kukinoa kikosi hicho kuanzia msimu ujao wa mashindano, ikiwemo Kombe la Shirikisho Afrika.
Juni 19, gazeti hili liliandika habari za klabu hiyo kuwa kwenye mazungumzo na kocha huyo ili kuja kuchukua mikoba ya Taoussi raia wa Morocco.
Ibenga, alisema jana moja ya mikakati atakayoifanyia kazi ni kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri kwenye mashindano ya Kimataifa.
"Naona fahari kupata nafasi ya kufanya kazi kwenye timu hii, Azam ni timu kubwa si Tanzania tu hata Afrika kwa ujumla, sijaja hapa kutangaza wasifu wangu, nimekuja kufanya kazi, nimekuja kuonyesha ujuzi wangu, hivyo nadhani tutafanya kazi pamoja, kazi hii siwezi kuifanya peke yangu, nahitaji ushirikiano," alisema.
Aliipongeza Azam kwa kufanikiwa kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu, akisema hii imewafanya kucheza michuano ya Kombe la Shirikisho msimu ujao, hivyo wamemrahisishia kazi, kwani anafika na kukiandaa kikosi kwa michuano ya kimataifa.
"Nampongeza kocha aliyepita, Rachid ni rafiki yangu sana, nadhani kinachotakiwa kufanyika msimu ujao ni kufanya vizuri tofauti na msimu huu," alisema Ibenge.
Alisema soka la Tanzania limekuwa na ushindani mkubwa, hasa kwa timu tatu za Simba, Yanga na Azam, hivyo amekuja kuifanya timu hiyo izidi kuwa tishio.
"Tanzania ina ushindani mkubwa kwenye ligi, kuna Simba, Yanga na sisi ni miogoni mwa timu tatu bora, nawaomba mashabiki watusapoti tufanye kazi pamoja ili tuifanikishe Azam kwenye malengo tunayokusudia," alisema.
Ibenge, ni mmoja kati ya makocha maarufu na wazoefu Afrika, akiwa ameipa ubingwa wa CHAN timu ya taifa ya Jamhuri ya Congo mwaka 2016, fainali zilizofanyika nchini Rwanda, akaipa ubingwa wa Kombe la Shirikisho klabu ya RS Berkane ya Morocco msimu wa 2021/22 na m,simu uliomalizika hivi karibuni aliifikisha Al Hilal ya Sudan hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kabla ya kusukumizwa na Al Ahly ya Misri.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED