Dhamira ya Serikali kutekeleza mradi mkubwa kuchakata, kusindika gesi asilia

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:57 AM Apr 30 2025
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk.Doto Biteko.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk.Doto Biteko amesema dhamira ya Serikali ni kutekeleza mradi mkubwa wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia (LNG) kutokana na faida zake kiuchumi ila kwa sasa kuna maeneo ambayo Serikali inayafanyia kazi kwa kina kupitia majadiliano na Wawekezaji ili mradi husika uwe na tija kwa nchi na wananchi.

Ameyasema hayo jana Aprili 29, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu hoja mbalimbali zilizotolewa na Wabunge kuhusu Hotuba ya Bajeti ya  Wizara ya Nishati ya shilingi Trilioni 2.2 kwa mwaka 2025/2026 kabla ya kupitishwa kwa kishindo na Bunge hilo kwa asilimia 100.


“Mradi wa LNG umeanza kusemwa kwa muda mrefu na kila mmoja angetamani mradi huu ukamilike jana lakini lazima tukubaliane kuwa lazima tujadiliane kwa kina na wawekezaji ili kupata kilicho bora na kuleta tija, ninachotaka kuwahakikishia ni kuwa timu ya majadiliano ya Serikali na Wawekezaji wanaendelea na majadiliano na tunatarajia kuwa ndani ya mwaka huu 2025 kama tutakuwa tumemaliza masuala matatu yaliyosalia kujadiliwa, mkataba huo utasainiwa ili mradi uanze mara moja.” alisema Dk.Biteko


Aliongeza kuwa, Rais, Dk.Samia Suluhu Hassan ana kiu ya kuona mradi huo  unaanza na alishatoa maagizo kwa Wizara ya kuhakikisha kuwa mradi unaanza kutekelezwa.

Akijibu hoja kuhusu vituo vya mafuta vinavyoongezeka na kujengwa kwa kukaribiana,Dk.Biteko amesema kuwa Wizara ya Nishati imeanza mazungumzo na Wizara ya Ardhi ili kuongeza umbali kati ya kituo kimoja na kingine kutoka mita 200 za sasa kwa lengo la kuleta usalama wa watu, mazingira na shughuli za kijamii.

Kuhusu msamaha wa kodi mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa gesi inayotumika kwenye vyombo vya moto kama vile magari (CNG), Dk. Biteko alisema kuwa Serikali ilishatoa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa vifaa na mashine mbalimbali zinazotumika katika mnyororo wa thamani kwa miradi ya CNG kama vile mitungi ya CNG pamoja na vifaa vya kuwezesha kufunga mfumo kuwezesha magari kutumia gesi hiyo.


Aliongeza kuwa, katika mwaka 2024/2025 Wizara ya Nishati imewasilisha Wizara ya Fedha mapendekezo ya maboresho ya kodi katika gesi asilia inayotumika kwenye magari ili kuzidi kuhamasisha matumizi ya CNG na wawekezaji wanaowekeza kwenye miradi hiyo wapate faida na kurudisha gharama wanazowekeza kwa haraka.

Akijibu  hoja za Wabunge kuhusu gharama za kuunganisha umeme vijijini na mijini, Dkt.Biteko amesema kuwa imeundwa timu kwa ajili ya kuangalia namna gani gharama hizo zitapunguzwa lengo likiwa ni kuleta unafuu kwa wananchi.

Kuhusu usambazaji wa umeme Vijijini, Dkt.Biteko amesema kuwa, Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan anapaswa kupongezwa kwa kufikisha umeme katika Vijiji vyote 12,318 kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 huku kazi ya kupeleka umeme vitongojini ikiendelea kwa kasi.

Akizungumzia ujenzi wa vituo vya kupoza umeme katika wilaya zote nchini kupitia mradi wa gridi imara, Dk. Biteko amesema kuwa tayari Serikali imeshanunua viwanja kwa ajili kujenga vituo hivyo na katika awamu ya kwanza vitajengwa vituo 14 huku utekelezaji ukiendelea na katika laini za umeme ambazo ni ndefu sana Serikali itaweka switching stations.

Aidha, kuhusu suala la kukatika kwa umeme nchini, Dk.Biteko amesema kuwa  limepungua kwa asilimia 48 huku dakika za kukatika umeme zikipungua kwa asilimia 64 na kwa sasa umeme ukikatika ni kwa sababu tu ya matengenezo ya miundombinu. Hata hivyo amesema Serikali inaendelea kuimarisha kituo cha huduma kwa  Wateja TANESCO ili taarifa ziwafikie wananchi kwa wakati pale umeme unapokatika ikiwemo kila wilaya kuwa na kundi sogozi.

Awali, wakati wa kuhitimisha Hotuba hiyo ya Wizara ya Nishati, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga alimpongeza Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya katika Taifa hususan kwenye Sekta ya Nishati akieleza kuwa moja ya misingi ya ukuaji wa kiuchumi na maendeleo katika Taifa lolote ni uwekezaji katika Sekta ya Nishati.


Akizungumzia mikoa ambayo bado haijaunganishwa katika gridi ya Taifa ya umeme, Kapinga alisema kuwa kuna miradi mbalimbali inayoendelea ambapo katika Mkoa wa Rukwa kuna mradi mkubwa wa kusafirisha umeme unaoendelea wa kutoka Iringa-Tunduma hadi Rukwa na kipande kingine cha mradi kitakachounganisha gridi ya Tanzania na Zambia.

“Mhe.Spika  katika Mkoa wa Mtwara na Lindi tayari mkandarasi yupo eneo la kazi, mradi umeanza kwa kujenga njia ya umeme kutokea Songea-Tunduru-Masasi hadi Mahumbika na tumeshaanza kulipa fidia katika eneo la Tunduru hadi Masasi takriban shilingi bilioni 4.6 na eneo lililobakia la Songea kuelekea Namtumbo na Tunduru tutaendelea kulipa fidia ya takriban shilingi bilioni 2.7.” alisema Kapinga


Kuhusu kupeleka gridi ya Taifa katika Mkoa wa Kagera alisema kuwa kazi inaendelea kupitia ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya Benaco-Kyaka na katika Mkoa wa Katavi mradi wa kupeleka umeme wa gridi mkoani humo uko katika hatua za mwisho.

Akizungumzia kazi ya kupeleka umeme kwenye visiwa mbalimbali nchini, Kapinga alisema kuwa, Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 9.89 ili kupeleka mifumo ya umeme jua katika visiwa 118 ambavyo vipo katika mikoa zaidi ya mitano hususan Wilaya ya Ukerewe.

Kuhusu maboresho miundombinu ya umeme katika Mkoa wa Dar es Salaam, Kapinga alieleza kuwa kuna kazi zinaendelea kwa lengo la kuwawezesha wananchi kupata umeme wa uhakika ikiwemo uboreshaji wa kituo cha Mbagala ambacho kilikuwa na transfoma yenye uwezo wa MVA 50 lakini sasa inawekwa transfoma mpya yenye uwezo wa MVA 120 ili kukiongezea uwezo kituo hicho ili wananchi wa Mbagala, Temeke, Yombo, Mkuranga na baadhi ya maeneo ya Kigamboni waendelee kupata umeme wa uhakika.

Alieleza kuwa kazi hiyo imefikia mwishoni na muda wowote transfoma hiyo itaanza kufanya kazi. Kwa eneo la Kigamboni amesema maboresho pia yanaendelea kufanyika na kwamba wananchi tayari wameshaanza kuona mabadiliko ya upatikanaji umeme kupitia maboresho hayo.