Diddy alitumia umaarufu wake kuwanyanyasa wanawake

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:05 AM May 13 2025
Sean "Diddy" Combs (55).
Picha:Mtandao
Sean "Diddy" Combs (55).

Mwanamuziki maarufu na mfanyabiashara mashuhuri, Sean "Diddy" Combs (55), anakabiliwa na mashtaka mazito yanayohusisha unyanyasaji wa kingono, ulaghai, usafirishaji wa watu kwa ajili ya ukahaba, na kuendesha mtandao wa uhalifu wa kijinsia. Mashtaka haya yamewasilishwa katika mahakama ya Marekani, na tayari yamezua mjadala mpana duniani kote.

Katika ufunguzi wa kesi hiyo, waendesha mashtaka walieleza kuwa Diddy alitumia umaarufu wake, hofu na vitisho vya vurugu ili kuwatawala wanawake – hasa wale waliokuwa wapenzi wake wa zamani – kwa kuwalazimisha kushiriki vitendo vya kingono bila ridhaa yao. Vitendo hivyo vilinaswa kwa video na kuhifadhiwa kwa matumizi binafsi.

Ushahidi muhimu katika kesi hiyo ni video inayomuonesha Diddy akimpiga na kumburuta kwa nywele mpenzi wake wa zamani, Cassandra Ventura, katika hoteli moja jijini Los Angeles mwaka 2016. Mlinzi wa hoteli hiyo amethibitisha uhalisia wa video hiyo, ambayo tayari imezagaa kwenye mitandao ya kijamii.

Mwendesha mashtaka Emily Johnson alidai kuwa Diddy aliwatumia wanawake kama vyombo vya starehe kupitia kile alichokiita “freak-offs” — tafrija za kingono zilizolenga udhibiti wa kisaikolojia na udhalilishaji wa kimwili.

Shahidi mwingine, Daniel Phillip, ambaye aliwahi kuwa meneja wa wasanii, alitoa ushahidi wa kushtua akisema kuwa alilazimishwa kushiriki tendo la ngono na Ventura kwa zaidi ya saa kumi huku Diddy akitazama na kurekodi tukio hilo. Phillip alisema hakuweza kutoa taarifa kwa polisi kwa hofu ya kuuawa au kutekwa, akieleza kuwa Diddy ni mtu mwenye "nguvu kubwa na ushawishi usio wa kawaida."

Aidha, Phillip alieleza kuwa aliwahi kushuhudia mara kadhaa Diddy akimshambulia Bi Ventura, na katika tukio moja alimvuta nywele kwa nguvu huku mwanamke huyo akipiga kelele kwa maumivu.

Hata hivyo, mawakili wa utetezi wa Diddy wamejibu kwa kusema kuwa video hiyo haithibitishi uwepo wa mtandao wa biashara ya ngono. Wakili Teny Geragos alisema, “Ni kweli video inaonyesha tabia isiyokubalika, lakini unyanyasaji wa majumbani si sawa na biashara ya ngono.”

Kesi hiyo inaendelea kushika kasi huku ikisubiriwa kwa hamu kusikilizwa tena Jumanne, ambapo Bi Cassandra Ventura anatarajiwa kutoa ushahidi wake mbele ya mahakama.