Wakulima wa korosho Nachingwea wafurahia pembejeo za ruzuku
By
Gideon Mwakanosya
,
Nipashe
Published at 02:56 PM May 13 2025
Picha: Mtandao
Korosho.
Wakulima wa zao la korosho katika vijiji vya Kiparamtuwa na Farmseventine wilayani Nachingwea, mkoani Lindi, wameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na Chakula kwa kuwapatia pembejeo za ruzuku aina ya Simba Sulphur Dust, kwa ajili ya kupulizia kwenye mashamba yao ya korosho.
Wakizungumza na waandishi wa habari katika kijiji cha Palamtua, wakulima hao wamesema kuwa msaada huo wa pembejeo ni hatua muhimu katika kuinua uzalishaji wa korosho na kuimarisha kipato chao.
Noel Mmole, mkazi wa kijiji cha Farmseventine, na Mwanahamisi Rashid, mkazi wa Palamtua, wameeleza kuwa dawa hizo za ruzuku zimekuwa mkombozi mkubwa kwa wakulima wadogo. Wameiomba serikali kuendeleza mpango huo kwa kuwa zao la korosho ni tegemeo kuu kwa maisha ya wananchi na chanzo muhimu cha mapato kwa serikali.
“Leo tumepokea Simba Sulphur Dust kwa ajili ya mashamba yetu ya korosho. Tunaamini dawa hii itasaidia sana kuongeza tija, na kwa upande wetu, itatuwezesha kupata kipato cha kulipa ada za watoto, kugharamia mahitaji ya familia na kuboresha maisha kwa ujumla,” alisema Mmole. 1
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha RUNALI, Odas Mpunga, alisema kuwa zaidi ya tani 300 za pembejeo zimesambazwa leo kwa wakulima wa korosho katika maeneo hayo, pamoja na viuatilifu zaidi ya lita milioni 16 kwa ajili ya kupulizia mashamba.
Mpunga alitoa wito kwa wakulima kuzitumia pembejeo hizo kwa uangalifu na ufanisi ili kuongeza uzalishaji wa zao la korosho, jambo litakalosaidia kuongeza mapato kwa wakulima na taifa kwa ujumla.
“Tunahamasisha wakulima wetu kutumia vizuri pembejeo walizopata. Lengo ni kuhakikisha korosho inazalishwa kwa ubora na kwa wingi zaidi, ili kuimarisha maisha ya wakulima na kuongeza pato la taifa,” alisema.
Mpango huu wa utoaji wa pembejeo kwa ruzuku ni sehemu ya juhudi za serikali kuinua kilimo cha korosho, ambacho ni miongoni mwa mazao ya kimkakati nchini Tanzania.