Dira 2050 yaundiwa mikakati ya kisheria kuifaikisha

By Restuta James , Nipashe
Published at 01:32 PM Oct 17 2025
Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu.
Picha: Mpigapicha Wetu
Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu.

Serikali imeeleza dhamira yake ya kutengeneza sheria rafiki za uwekezaji zitakazoiwezesha kufikia uchumi wa kati wa juu kama ilivyobainishwa kwenye Dira 2050.

Ili kufikia uchumi huo, Dira 2050 imeweka lengo la kuchochea ukuaji wa Pato la Taifa kutoka Dola za Marekani bilioni 88.4 za sasa mpaka Dola trilioni moja, ifikapo mwaka 2050.

Hayo yamesemwa Alhamisi, Oktoba 16, 2025 wakati wa kikao kazi kati ya Ofisi ya Msajili wa Hazina, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria, kilichofanyika Kibaha, mkoani Pwani.

Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amesema maagizo waliyopewa na Rais Samia Suluhu Hassan, ni uboreshwaji wa sheria, ili ziendane na maono yaliyomo kwenye Dira 2050.

“Tunapaswa kuwa na sheria ambazo zitaongeza ufanisi wa taasisi za umma. Tunapaswa kuwa na sheria ambazo zitatoa wigo kwa sekta za umma kufanya kazi kwa ukaribu na sekta binafsi,” amesema Mchechu.

Amesema ufanisi wa sekta za umma, utaongeza mchango wake kwenye mapato ya ndani ya serikali kutoka asilimia nne ya sasa hadi 10, miaka minne ijayo, kama ilivyoelekezwa na Rais Samia. 

“Tunapaswa kuboresha huduma na bidhaa zetu, pamoja na kupunguza matumizi yasiuyokuwa ya lazima, ili kuongeza mapato na hatimaye gawio kwa serikali,” amesema.

Mchechu amesema serikali inataka kuona tija katika uwekezaji wake wa Sh. trilioni 92.3 ilioufanya katika taasisi za umma na kampuni ambazo ina umiliki wa hisa chache.  

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Samwel Maneno, amesema kuwa uimara wa taasisi za umma na sekta binafasi unategemea ubora wa sheria zinazosimamia uwekezaji.

Amesema kuwa usimamizi wa mikataba ya uwekezaji usipokuwa mzuri, itakuwa ngumu au itachukua muda mrefu kufikia matarajio yaliyowekwa na serikali.

Aidha, ametoa rai ya kuepuka urasimu usiokuwa wa lazima ili wawekezaji hasa katika eneo la ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).

Kwa upande wake Wakili Mkuu wa Serikali, Dk. Ally Possi, amesema sheria za nchi hazitakiwa ziwe kikwazo kwa wawekezaji, badala yake kivutio.

Aidha, amesema taasisi za umma zina jukumu la kutoa gawio na kukuza Uchumi wa nchi.

“Lakini hili haliwezi kutimia ikiwa taasisi hizo zitagubikwa na kesi ambazo zitazilazimu kulipa fedha baada ya hukumu ya mahakama kutolewa, na ni katika muktadha huo tumekutana kujadili namna bora ya kukabiliana na mapungufu ya kisheria,” amefafanua Dk. Possi.

Naye Mwandishi Mkuu wa Sheria Bw. Onorius Njole alisema kufikia uchumi wa Dola za Marekan trilioni moja, unategemea uimara wa taasisi za umma pamoja na mfumo imara wa kisheria katika eneo la uwekezaji.

“Ni lazima mashirika ya umma yasimamiwe na sheria za uwekezaji ambazo zinaendana na mahitaji ya sasa,” amesema.