Mgombea wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema kudumisha amani ni jukumu la kila mwananchi anayependa maendeleo na ustawi wa taifa.
Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo wakati alipojumuika na waumini wa dini ya Kiislamu katika Sala ya Ijumaa na Dua Maalum ya kuiombea nchi na uchaguzi mkuu, iliyofanyika katika Msikiti wa Muembe Shauri, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Amesema suala la amani si jukumu la mtu mmoja au kundi fulani, bali ni wajibu wa kila raia kuhakikisha utulivu unaendelea kuwepo, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
“Amani ndiyo nguzo kuu ya maendeleo. Bila amani hakuna umoja, na bila umoja hakuna maendeleo. Ni jukumu letu sote kuilinda,” amesema Dk. Mwinyi.
Ameeleza kuwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta mbalimbali kwa kipindi cha miaka minne iliyopita yametokana na kuwepo kwa amani, hali iliyowezesha Serikali kutekeleza mipango yake ya maendeleo kikamilifu.
Aidha, Rais Mwinyi ametoa wito kwa wananchi kuwa waangalifu na kauli zao, akibainisha kuwa vurugu hazianzi kwa bunduki, bali kwa maneno au vitendo vya mtu vinavyoweza kuchochea mgawanyiko na chuki.
“Ni muhimu kila mmoja wetu achunge kauli na matendo yake. Tuhubiri amani, tuilinde amani, na tuihifadhi amani yetu,” amesisitiza Dk. Mwinyi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED