Viongozi wa dini Mara watoa wito wa kudumisha amani kipindi cha uchaguzi

By Neema Emmanuel , Nipashe
Published at 05:49 PM Oct 17 2025
azaro Nyalandu.

Viongozi wa dini mkoani Mara wameiomba jamii kudumisha amani katika kipindi hiki cha uchaguzi na kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili kuchagua viongozi watakaowaletea maendeleo katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Wakizungumza kuhusu maandalizi ya uchaguzi, viongozi hao wamesema kumekuwepo na watu wachache wanaosambaza taharuki miongoni mwa wananchi kuhusu zoezi la uchaguzi. Wameitaka Serikali kuchukua hatua za kuzuia vitendo hivyo na kuwalinda wananchi wake dhidi ya watu wanaoweza kuhatarisha amani.

Akieleza umuhimu wa kudumisha amani, aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amesema msingi wa umoja na mshikamano wa taifa ni jamii kuishi kwa upendo na amani. Amehimiza viongozi wa dini kuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu kwa waumini juu ya umuhimu wa kujitokeza kupiga kura ili kutimiza haki yao ya kidemokrasia.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Canal Evance Mtambi, amesema majukumu makuu ya vyombo vya ulinzi na usalama ni kulinda raia pamoja na mali zao, na kuhakikisha mipaka ya nchi inabaki salama. Amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuepuka vitendo vyovyote vya uvunjifu wa amani na badala yake wakumbatie umoja na mshikamano wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu