Serikali yatoa magodoro kwa wanaowalea watoto waliotelekezwa mitaani

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 07:29 PM Oct 17 2025
Ofisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Kahama, Hamisi Mnumbi akiongea na watu wa kuaminika katika jamii kabla ya kuwakabidhi magodoro yaliyotolewa na serikali.
PICHA; SHABAN NJIA.
Ofisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Kahama, Hamisi Mnumbi akiongea na watu wa kuaminika katika jamii kabla ya kuwakabidhi magodoro yaliyotolewa na serikali.

Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga imeanza kampeni maalum ya kupambana na ukatili kwa watoto wanaoishi mazingira magumu kwa kushirikiana na watu wa kuaminika katika jamii, ikiwa ni hatua sahihi ya kuboresha mazingira ya malezi kwa watoto hao.

Ofisa Maendeleo ya Jamii Manispaa hiyo, Hamisi Mnumbi ameyabainisha haya leo wakati akikabidhi magodoro kwa watu wa kuaminika katika jamii yaliyotolewa kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kuwahifadhi watoto wanaopatikana mitaani baada ya kutelekezwa. 

Amesema, kazi wanazozifanya watu hao zilipaswa kufanywa na serikali lakini kwa mapenzi mema waliyonayo wamesaidia kupunguza wimbi la watoto wa mitaani hususani wale wanaotekelezwa hivyo wanawaunga mkono kwa kuwapatia msaada wa magodoro. 

Aidha Mnumbi amewataka kuwa waminifu kipindi chote cha malezi ya watoto hao wakati serikali ikiendelea kuwatafuta wazazi wao ili wawakabidhi nasio kuwafanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na kusisitiza madogoro hayo kutumika katika matumizi yaliyopangwa nasio vinginevyo. 

Ofisa Ustawi wa Jamii Abrahaman Nuru amesema, wamewatambua watu wa kuaminika kila kata na kuwapatia mafunzo maalumu juu ya vitendo vya ukatili wa kijinsia, kwani wamekuwa wakipokea watoto wengi wanaotelekezwa vituo vya mabasi na sehemu mbalimbali. 

Mwenyekiti wa Watu wa kuaminika katika jamii, Flora London amesema, walikuwa wakiwapata watoto mitaani lakini hawakuwa na sehemu ya kuwalaza ila kwasasa wameondokana na adha hiyo baada ya kila mmoja wao kupatiwa godoro. 

Amesema, hivi karibuni alimpokea mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 15 aliyepotea na baada ya mahojiano alibaini alikuwa mjamzito na ametoroka kwani Morogoro Ifikala, lakini mama yake ameshapatika yupo katika kijiji cha Chela na muda wowote atafika kumchukua. 

Ofisa mradi wa Huduma za Ustawi wa Jamii vituo vya mabasi kutoka Shirika la Railway Children Africa (RCA) Renatus Faustine amesema, lengo la kushirikiana na watu wa kuaminika ni kuondoa wimbi la watoto wanaishi na kufanyakazi mitaani. 

Amesema, baada ya wazazi wao kupatikana wamekuwa wakisafirisha mpaka katika makazi yao ndani na nje ya Tanzania na wamekuwa wakiwarejesha kwa kushirikiana na maofisa ustawi wa jamii katika mikoa ya Mwanza, Geita, Shinyanga, Kahama, Tabora, Kagera na Dodoma.