Watoto 11 wenye utapiamlo watoroshwa matibabu, hawajulikani walipo

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 07:36 PM Oct 17 2025
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama, Glory Absalum akizungumza wakati wa kikao cha lishe cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/26.
PICHA; SHABAN NJIA.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama, Glory Absalum akizungumza wakati wa kikao cha lishe cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/26.

Watoto 11 wenye ugonjwa wa utapiamlo katika halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga, wanadaiwa kutoroshwa na wazazi wao baada ya kushindwa kumdu gharama za kuishi hospitalini wakati watoto wao akiendelea kupata matibabu yanayochukua muda siku saba mpaka 21.

Ofisa Lishe wa Halmashauri ya hiyo, Mohamed Mkoko ameyabainisha  haya leo katika kikao cha lishe cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/2026 kilichofanyika shule ya sekondari Kisuke. 

Amesema, walipokea na kuwahudumia watoto 22 wenye ugonjwa wa utapiamlo kati yake nane walitoka nje ya halmashauri ambapo sita wanatoka mkoa wa Tabora na wawili mkoani wa Kagera, 14 walitoka ndani ya halmashauri na kati yake wawili walipona na mmoja alifariki kabla ya kuanza matibabu yake. 

Mkoko amesema, watoto 11 wenye ugonjwa huo walitoroshwa matibabu na wazazi wao na wamewatafuta na hawakufanikiwa kupata taarifa za mahali walipo na hawafahamu kama bado wazima au wamesha kufa na sababu kubwa ni wazazi kushindwa kujilea wakati watoto wakipatiwa matibabu. 

“Matibabu ya mtoto mmoja mwenye utapiamlo serikali inatumia Sh.267,500 kwa kipindi ambacho mtoto anakuwa wodini ambapo wanakaa wastani wa siku saba mpaka 21 hivyo muda wote huo mzazi anatakiwa kujilea na anaposhindwa hutokomea na mtoto kusikojulikana”Ameongeza Mkoko.

 Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama, Glory Absalum amesema, si rahisi wananchi hususani wanaotoka vijijini kumudu gharama za kujihudumia mwenyewe wakati mtoto wake akiendelea kupata matibabu kwa muda wote huo na ndio sababu asilimia 79 wamekimbia matibabu ya watoto wao.

 Amesema, namna sahihi ya kutatua tatizo hilo ni kuwa na sehemu ya ulekebishaji wa afya katika hospitali ya wilaya na itapunguza tatizo kwa kiwango kikubwa na wananchi watapunguziwa gharama za kujihudumia wenyewe kwa serikali kusaidia baadhi ya gharama.