Mgombea Mwenza wa Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi amesema Rais Samia Suluhu Hassan katika uongozi wake amefanikiwa kuvijenga na kuviimarisha vyombo vya ulinzi na usalama kuliko wakati mwingine wowote.
Amesema majeshi ya ulinzi na usalama yameongezewa askari, mafunzo ya ndani na nje, vitendea kazi pamoja na mafunzo ya uhusiano mzuri na raia.
Amesema haya leo Oktoba 17 wilayani Kondoa mkoani Dodoma wakati akihutubia wananchi wa wilaya hiyo ikiwa ni mwendelezo wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu.
Balozi Dk. Nchimbi amesema: " Katika miaka minne ya uongozi wake, Rais Samia amefanikiwa kuendeleza amani, usalama na utangamano katika nchi yetu. Na amefanikiwa kwa kutengeneza mazingira mazuri ya uhusiano kati ya wananchi, lakini vilevile amefanikiwa kwa kuvijenga na kuviimarisha vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kuliko wakati mwingine wowote".
Amesema: "Majeshi yetu yote ya ulinzi na usalama yameongezewa idadi ya askari kwa maelfu, lakini pia yameongeza mafunzo ndani na nje ya nchi, lakini pia wameongezewa vitendea kazi, lakini pia wamepata mafunzo ya uhusiano yao na raia. Hivyo majeshi yetu sasa ni imara zaidi kuliko wakati mwingine wowote katika historia yetu".
Dk. Nchimbi amesema Rais Samia Suluhu Hassan anastahiri kuchaguliwa tena kwa miaka mitano ijayo kutokana na mambo makubwa aliyoyatekeleza ndani ya muda mfupi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED