Miili ya vijana wanne imeokotwa Kibaha yenye dalili za mauaji

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 03:07 PM Oct 17 2025
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase.
Picha: Mpigapicha Wetu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase.

Miili ya vijana wanne wenye umri wa miaka 19 hadi 21 imeokotwa pembezoni mwa barabara ya Mapinga, Kibaha, ikiwa na majeraha usoni na miguuni, ikibainika kuwa tukio hilo linaashiria mauaji.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, amesema awali walipokea taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Kidimu kuhusu kuonekana kwa miili hiyo isiyojulikana. Baada ya kupokea taarifa, Polisi wakiwa na wataalamu wa uchunguzi wa matukio makubwa walifika eneo la tukio na kukuta miili yote wakiwa wanaume.

Miili hiyo imetambuliwa na ndugu zao; watatu kati yao ni deiweka (day worker) wa boda boda, na mmoja ni dereva wa bajaji. Kamanda Morcase amesema waliotambuliwa ni:

  • Mikidadi Abas (21), mkazi wa Tabata Chang’ombe
  • Hassan Jumanne (21), mkazi wa Tabata Chang’ombe
  • Fadhili Patricia (19), mkazi wa Vingunguti Miembeni, deiweka wa boda boda
  • Abdallah Fadhili (21), mkazi wa Kisulu Tabata, dereva wa bajaji

Miili yote imefikishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Tumbi kwa uchunguzi zaidi, na baadaye imikabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi.

Kamanda Morcase ameongeza kuwa uchunguzi wa kina unaendelea ili kubaini wahusika wa mauaji hayo na kubaini wakati na sababu za tukio hilo.