Mgombea urais kupitia Chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo, ametoa wito kwa Watanzania kudumisha amani kabla na baada ya uchaguzi mkuu ujao, akisisitiza kuwa amani ndiyo nguzo kuu ya maendeleo ya taifa lolote duniani.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana katika muendelezo wa kampeni za chama hicho zinazofanyika kwa mtindo wa “mobile kampeni”, Doyo alisema NLD imekuwa ikifanya kampeni za kistaarabu na kisayansi katika mikoa 26 nchini hadi sasa.
Alieleza kuwa kampeni hizo zimekuwa zikilenga kufikia wananchi moja kwa moja, kuwapa elimu ya sera za chama na kuelewa changamoto wanazokabiliana nazo, bila kutumia lugha ya kejeli au kudhalilisha watu wengine.
“Niwaombe sana Watanzania wenzangu, mkapige kura kwa amani. Mkivunja amani, hakuna maendeleo yatakayopatikana. Amani ndiyo tunu ya taifa letu,” alisema Doyo.
Aidha, alisisitiza kuwa amani ni sharti muhimu la maendeleo, na pale ambapo amani ipo, ndipo serikali yoyote inaweza kutekeleza kwa ufanisi ahadi zake kwa wananchi, ikiwemo kuboresha huduma za jamii, kukuza uchumi na kuongeza ajira.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED