Jeshi la Polisi mkoani Geita linamshikilia Martha Japhet (44), mkulima na mkazi wa Kitongoji cha Mzalendo, Kijiji cha Mawemeru, Kata ya Nyarugusu, Wilaya ya Geita, kwa tuhuma za kumuua mume wake Shabani Paschal (55), ambaye alikuwa mkulima na mchimbaji wa madini.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, akieleza kuwa lilibainika Oktoba 16, 2025, saa saba mchana, baada ya jeshi hilo kupokea taarifa za kutoweka kwa marehemu tangu Oktoba 11, mwaka huu.
“Baada ya kupokea taarifa hizo, askari walifanya uchunguzi wa awali na kumkamata mtuhumiwa ambaye alikiri kuhusika na mauaji hayo,” amesema Kamanda Jongo.
Amefafanua kuwa katika mahojiano, mtuhumiwa alieleza kuwa alimshambulia mume wake kwa kitu chenye ncha kali sehemu ya kichwani, na baada ya kubaini amefariki dunia, alichimba shimo ndani ya chumba walichokuwa wanalala, akamzika, kisha akafunika kwa udongo na magunia ya mihogo (udaga) ili kuficha ushahidi.
Kamanda Jongo amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni migogoro ya kifamilia, na kwamba jeshi hilo linaendelea na uchunguzi zaidi kabla ya mtuhumiwa kufikishwa mahakamani.
Aidha, amewataka wananchi kuepuka kujichukulia sheria mikononi mwao na kutoa taarifa mapema kwa vyombo vya usalama pindi wanapoona viashiria vya migogoro au ukatili wa kifamilia ili hatua zichukuliwe kwa haraka.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED