Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli, imesema kuwa utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu miradi inayotarajiwa kutekelezwa ni miongoni mwa masuala muhimu ya kuzingatia ili kufanikisha utekelezaji wa miradi hiyo kwa ufanisi.
Mjiolojia Mwandamizi kutoka Mamlaka hiyo Ebeneza Mollel, ametoa kauli hiyo katika Kijiji cha Ruvula Mkoani Mtwara, wakati wa kazi ya utoaji wa elimu ya mradi wa uchimbaji wa visima vitatu vya gesi asilia unaotarajiwa kutekelezwa katika Kitalu cha Mnazi Bay kilichopo Mkoani humo.
Mollel amesema kuwa, pamoja na kudhibiti shughuli za kitalaamu, Mamlaka hiyo, inahakikisha wananchi wanajengewa uelewa wa miradi kabla ya kuanza utekelezaji.
“Sisi kama Mamlaka tunahakikisha kuwa, jamii zinazoishi au zinazozunguka maeneo ambayo miradi ya mkondo wa juu wa petroli inatekelezwa, zinashirikishwa kikamilifu katika miradi hiyo na kujengewa uelewa wa kina kuhusiana na mradi” amesema Mollel.
Sambamba na hilo, Mollel amesema kuwa, Mamlaka hiyo inafuatilia kwa karibu hatua zote za utekelezaji wa mradi wa uchimbaji wa visima vya gesi asilia na kuwakumbusha watekelezaji wa mradi umuhimu wa utoaji wa uelewa wa mradi kwa wananchi.
Amesema kazi ya utoaji wa elimu kuhusu mradi wa uchimbaji wa visima vya gesi asilia katika Kitalu cha Mnazi Bay linafanywa katika vijiji vitatu ambavyo ni Ruvula, Msimbati na Mtandi vilivyopo katika Kata ya Msimbati, Mtwara.
Mradi huo unahusisha uchimbaji wa visima viwili vya uzalishaji na kisima kimoja cha utafiti unatarajiwa kugharimu zaidi ya Dola za Marekani milioni 80.2.
Utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuanza Desemba mwaka huu ambapo utawezesha, pamoja na mambo mengine, ongezeko la uzalishaji wa gesi asilia kwa wastani wa futi za ujazo milioni 30 kwa siku.
Ongezeko hilo litasaidia upatikanaji wa gesi asilia kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kuzalisha umeme, kwenye viwanda, majumbani na kwenye vyombo vya usafiri (magari na bajaji).
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED