Samia kutua kesho Katavi, Balozi Migiro asafisha njia

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 07:04 PM Oct 17 2025
Samia kutua kesho Katavi,  Balozi Migiro asafisha njia.
Picha: Mpigapicha Wetu
Samia kutua kesho Katavi, Balozi Migiro asafisha njia.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Asha-Rose Migiro, amefanya kikao kazi na wajumbe wa Sekreterieti ya CCM Mkoa wa Katavi, kilichofanyika mjini Mpanda, leo Ijumaa, Oktoba 17, 2025.

Kikao hicho, ambacho kilihudhuriwa pia na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Katavi, Idd Kimanta, na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa, Gilbert Sampa, ni sehemu ya maandalizi ya kampeni za mgombea urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan.

Dk. Samia anatarajiwa kuendelea na kampeni zake mkoani Katavi kesho Jumamosi, baada ya kuhitimisha ziara yake mikoa ya Kanda ya Ziwa jana, katika Mkoa wa Kagera, ambapo maelfu ya wananchi walihudhuria.

Wananchi wa Katavi wameeleza hamasa yao kubwa ya kumpokea kiongozi huyo.

“Tumepanga kumpokea kwa wingi. Tumejiandaa kusikiliza sera atakazotoa ili tuweze kuchagua kiongozi sahihi atakayetuongoza kwa maono na kukuza uchumi wa nchi na wa kila mmoja,” amesema Neema Mwakitalu, mkazi wa Mpanda.

Aidha, Shabani Mlozi, mkazi wa Mpanda, amesema wanajipanga mapema kufika uwanjani ili kumsikiliza Dkt. Samia akieleza mipango yake ya kuimarisha kilimo na miundombinu mkoani Katavi.