IGP Wambura amzawadia askari aliyoumia kazini bajaji mpya

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 04:06 PM Oct 17 2025
IGP Wambura amzawadia askari aliyoumia kazini bajaji mpya.
Picha: Mpigapicha Wetu
IGP Wambura amzawadia askari aliyoumia kazini bajaji mpya.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga, amemkabidhi Bajaji mpya Koplo Anna Lufingo kutoka Wilaya ya Mbeya, kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Camillus Wambura.

Bajaji hiyo imetolewa Oktoba 17, 2025 kwa lengo la kumrahisishia usafiri wa kwenda na kurudi kazini, baada ya Koplo Anna kupata ulemavu wa mguu kufuatia ajali alipokuwa akitekeleza majukumu yake ya kazi.

Licha ya changamoto hiyo, Koplo Anna ameendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi, uadilifu na uaminifu mkubwa katika Kituo cha Polisi Iyunga, jijini Mbeya — jambo lililowagusa viongozi wake na kupelekea kupokea heshima hiyo kutoka kwa IGP Wambura.

“Tumevutiwa na moyo wa kujituma wa askari huyu licha ya hali yake ya kiafya. Huu ni mfano wa kuigwa kwa askari wengine,” amesema Kamanda Kuzaga akimkabidhi zawadi hiyo.

Ikumbukwe kuwa huu ni msaada wa pili kutolewa na IGP Wambura kwa askari wa Mkoa wa Mbeya waliopata ajali kazini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Jeshi la Polisi kutambua na kuthamini mchango wa askari wanaotekeleza majukumu yao kwa moyo wa kujitolea.