Dk. Kilabuko: Ushirikiano wa kikanda muhimu kukabili maafa ya kibinadamu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:55 PM Jul 10 2025

Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dk. James Kilabuko.
Picha: Mpigapicha Wetu
Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dk. James Kilabuko.

Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dk. James Kilabuko amehimiza ushirikiano wa kikanda katika kukabiliana na majanga ya kibinadamu yanayochochewa na mabadiliko ya hali ya hewa, kwa lengo la kubadilishana uzoefu wa kitaalamu na kuimarisha vituo vya ufuatiliaji wa majanga na tahadhari ya mapema (Situation Room).

Akizungumza leo wakati wa ufunguzi wa mafunzo maalum ya kubadilishana uzoefu, yaliyoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na UNDRR na Kituo cha Sayansi cha Afrika Magharibi kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (WASCAL), Dk. Kilabuko amesema mafunzo hayo ni sehemu ya kuimarisha uwezo wa kanda katika kukabili matukio ya majanga. Mafunzo hayo yalihusisha ujumbe kutoka Ghana, Togo na Burkina Faso.

Dk. Kilabuko ameeleza kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa majanga, kupitia vituo vyenye uwezo wa kukusanya taarifa mbalimbali, zikiwemo za hali ya hewa, maji, kijamii na kiuchumi, jambo linalosaidia kukabili majanga kama vile ukame na mafuriko.

 “Tunauzoefu mkubwa wa kiutendaji ambao unasaidia kuhakikisha vituo vyetu vinafanya kazi kwa ufanisi kwa kuratibu taasisi mbalimbali kukabiliana na majanga,” amesema Dk. Kilabuko.

1