Dk. Kimambo aanza na weledi kwa watumishi MNH

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 04:46 PM Jun 27 2025
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Delilah Kimambo
Picha: MNH
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Delilah Kimambo

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Delilah Kimambo, amewataka watumishi wa ustawi wa jamii hospitalini hapo kuzingatia weledi na kuonyesha moyo wa huruma na upendo wakati wa kuwahudumia wateja wanaofika kupatiwa huduma katika ofisi zao

Dk. Kimambo ameyasema hayo leo, Juni 27, 2025, wakati wa kikao cha pamoja na wafanyakazi wa idara hiyo, ikiwa ni sehemu ya mpango wake wa kuboresha mawasiliano ya ndani na kufanikisha uwajibikaji na uwazi katika utoaji wa huduma.

Watumishi wa MNH wahimizwa weledi wakitoa huduma

"Tujishushe kwenye viwango vya hawa watu, tuwahudumie kwa kujali na kwa upendo. Tutajua kwa kina shida zao na jinsi ya kuwasaidia kuendana na mahitaji yao. Nyie ni kitengo muhimu sana, nyie ndio watetezi wa wateja wetu, mnatakiwa kuwa sauti yao pale wanapokosa nguvu, na kuwa faraja yao pale wanapokata tamaa," amesema Dk. Kimambo.

Ustawi wa jamii katika hospitali imekuwa kimbilio huku wakipokea maoni utoaji msaada kwa wagongwa
Dk. Kimambo amewahimiza wahudumu hao kushirikiana kwa karibu na idara nyingine, akisisitiza kuwa mafanikio ya hospitali yanategemea mshikamano na moyo wa kuwahudumia wananchi kwa pamoja.
Dk. Kimambo (kushoto) ameteuliwa hivi karibuni kuwa Mkurugenzi Mtendaji MNH
Mkurugenzi wa Huduma za Ukunga na Uuguzi MNH, Redemptha Matindi, amemshukuru Dk. Kimambo, kwa kutenga muda kuzungumza na wafanyakazi hao, na kusisitiza kuwa kurugenzi yake itaendelea kuzingatia maelekezo na ushauri uliotolewa ili kuhakikisha MNH inabaki kuwa kimbilio la kila mmoja.