Dk. Mwinyi aahidi kuimarisha barabara,elimu Zanzibar

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 11:16 AM Oct 02 2025
Mgombea wa Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Mgombea wa Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kuendeleza na kuimarisha miundombinu ya barabara pamoja na sekta ya elimu ili kuchochea maendeleo ya Unguja na Pemba.

Akihutubia wananchi wa Jimbo la Pangawe, Mkoa wa Mjini Magharibi, Oktoba 1, Dk. Mwinyi alisema serikali atakayoiongoza itaongeza mtandao wa barabara za kisasa katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar ili kurahisisha usafiri na biashara za wananchi.

Aidha, aliahidi kuendelea na mpango wa ujenzi wa shule za ghorofa, hatua itakayosaidia kuondoa changamoto ya wanafunzi kusoma kwa zamu mbili (asubuhi na jioni), na badala yake kutoa mazingira bora ya elimu kwa wakati sahihi.

Dk. Mwinyi alisisitiza kuwa dhamira yake ni kuhakikisha Zanzibar inasonga mbele kimaendeleo kwa kugusa maisha ya kila mwananchi kupitia miradi ya elimu, miundombinu, huduma za jamii na uchumi.

“Tunataka Zanzibar yenye maendeleo makubwa – Unguja na Pemba – ambapo kila mwananchi atafaidika na fursa za kijamii na kiuchumi,” alisema Dk. Mwinyi.

Kwa upande wao, wananchi wa Pangawe wameeleza matumaini makubwa kwamba ahadi hizo zikitekelezwa zitabadilisha maisha yao ya kila siku na kuongeza ustawi wa jamii.