Dk Samia: Nitajenga barabara Ubena- Bigwa, Kisaki- Ngerengere

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:22 PM Aug 29 2025
Mgombea urais wa kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mgombea urais wa kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan.

Mgombea urais wa kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, amewahakikishia wananchi wa Morogoro kuwa barabara za Bigwa, Mvua - Kisaki zitakwenda kujengwa kwa kiwango cha lami.

Pamoja na barabara hiyo, amewatoa hofu kuwa hata barabara ya Ubena Zomozi hadi Ngerengere itajengwa pia, ili kumaliza changamoto hizo, akiwataka kuwa na imani na Chama Cha Mapinduzi.

Dk. Samia ameeleza hayo Ijumaa wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Ngerengere mkoani ikiwa ni siku ya pili ya mwendelezo kampeni za kusaka kura za uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29,2025.

Jana wakati akizindua kampeni zake uwanja wa Tanganyika Packers jijini Dar es Salaam alitoa ahadi mbalimbali ikiwemo kuwahikikishia matibabu bure kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na magonjwa yasiyoambukizi ya figo na saratani, mambo atakayoyafanya pindi atakaposhika madaraka Oktoba.

Uamuzi wa Dk Samia  wa kujega barabara hizo utakapokelewa kwa shangwe na wananchi wa Morogoro akiwemo mgombea ubunge wa Jimbo la Morogoro Kusini-Mashariki, Hamis Taletale
‘Babu Tale’ ambaye kwa nyakati tofuti amekuwa akitoa kilio cha miundombinu hiyo.

Amesema kwa sasa ujenzi barabara ya Ubena-Zomozi hadi Ngerengere yenye urefu wa kilomita 11.6 umefikia asilimia 24, akiwahakikishia atakwenda kuimalizia.

“Nafahamu uwa wakazi wengi katia halmashauri hii (Morogoro Vijijini) ni wakulima wazuri ingawa kuna kilio cha ardhi, ambacho tumekichukua tunakwenda kukifanyia kazi,”amesema Dkt Samia.

Ameongeza kuwa, “Barabara ya Bigwa, Mvua –Kisaki kila Babu Tale anaponiona, nimesema mimi ni mkazi wa eneo hilo, nitakapomaliza kipindi changu, nitakuwa natembelea eneo hilo kwa sababu nina mashamba.  Barabara hii ni muhimu kwetu tunakwenda kuijenga,”

“Hii bi barabara muhimu sana kwa sababu ndio inayounganisha maeneo mbalimbali na makao makuu ya halmashauri ya wilaya. Ahadi yangu na CCM kwa kuzingatia mahitaji ya maeneo haya, tunaahidi kujenga barabara ya Bigwa, Mvua-Kisaki na Ubena, Zomozi hadi Ngerengere,” amesema Dkt Samia huku akishangiliwa na wananchi waliohudhuria mkutano huo.