Wananchi wa Kijiji cha Langai, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, wameeleza kukabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa maji, hali inayowalazimu kutembea zaidi ya kilomita 10 kila siku kutafuta maji ya mifugo yao, huku wakihatarisha maisha kutokana na wanyama wakali kama tembo.
Wakizungumza Agosti 28, katika hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa tuta, wananchi hao walisema mbali na adha ya kutembea umbali mrefu, wamekuwa wakikumbana na vifo vya ghafla vya mifugo na hata kujeruhiwa na wanyama wa porini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Pangani, Segule Segule, alisema maboresho ya bwawa katika eneo hilo yameanza ili kuhakikisha upatikanaji wa maji unakuwa wa kudumu.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Fakii Lulandala, alisema Serikali imetoa zaidi ya shilingi milioni 700 kwa ajili ya kuboresha mradi wa maji ili kuondoa kero hiyo kwa wananchi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED