Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dk. Mustapher Mohamed Siyani, amewataka Majaji wa Mahakama Kuu nchini kuhakikisha wanashughulikia mashauri ya uchaguzi kwa weredi na haki ili kurejesha na kuimarisha imani ya wananchi kwa Mahakama.
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa Mafunzo ya Namna Bora ya Uendeshaji wa Mashauri ya Uchaguzi, Dk. Siyani amesema jamii imekuwa ikitoa malalamiko dhidi ya taasisi za umma ikiwemo Mahakama, jambo linaloathiri mtazamo wa wananchi kuhusu utoaji wa haki.
“Tunafahamu tarehe 29 Oktoba, 2025 kutakuwa na Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani. Tunapojiandaa kupokea na kusikiliza mashauri ya uchaguzi, ni lazima tufanye kazi kwa namna itakayohakikisha haki inapatikana na kuimarisha imani ya wananchi kwa Mahakama. Hili ni jambo la msingi sana,” amesema Dk. Siyani.
Amesisitiza kuwa Mahakama ndiyo chombo pekee chenye kauli ya mwisho kwenye utoaji haki kwa mujibu wa Ibara ya 107A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo ni wajibu wake kusikiliza na kutoa maamuzi kwa haki kwenye mashauri yote yatakayotokana na uchaguzi mkuu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED