Samia ahidi matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza kwa wasio na uwezo

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 11:01 AM Aug 29 2025
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan.

Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuwa endapo atapewa ridhaa ya kuendelea kuongoza nchi, serikali yake ndani ya siku 100 za mwanzo itaanza kugharamia matibabu na vipimo vya kibingwa kwa wananchi wasio na uwezo wanaougua magonjwa yasiyoambukiza.

Akizungumza leo katika uzinduzi wa kampeni za CCM uliofanyika katika viwanja vya Tanganyika Parkers, Dar es Salaam, mbele ya maelfu ya wananchi, Samia amesema magonjwa hayo ni pamoja na saratani, moyo, sukari, figo, mifupa na mishipa ya moyo, ambayo gharama zake ni kubwa na huchangia changamoto kwa familia nyingi zisizo na uwezo kifedha.

“Haya ndiyo magonjwa yenye gharama kubwa ambayo wananchi wasio na uwezo hushindwa kumudu gharama zake,” alisema Samia.

Aidha, ili kuimarisha huduma za afya nchini, Samia ameahidi serikali yake itaajiri wahudumu wapya wa afya 5,000 ndani ya siku 100 za mwanzo, wakiwemo wauguzi na wakunga, ili kuongeza nguvu kazi na kuboresha huduma hususan za afya ya mama na mtoto.