Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mobhare Matinyi, amempongeza mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Dk. Samia, iliyopo mkoani Dodoma, Miriam Shangali, kwa kushinda tuzo ya kimataifa ya Young Courage Award 2025. Hafla ya utoaji wa tuzo hiyo ilifanyika Agosti 27, 2025 jijini Stockholm.
Akizungumza na mwanafunzi huyo ubalozini Stockholm, Balozi Matinyi alisema ushindi huo ni heshima kubwa kwa taifa, akimpongeza Miriam kwa kuonesha ubunifu, juhudi, huruma na uongozi kwa wanafunzi wenzake nchini Tanzania, hatua iliyomfanya kutambuliwa kimataifa. Miriam alikuwa kijana pekee kutoka barani Afrika aliyepokea tuzo hiyo mwaka huu.
Miriam, ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha sita anayesomea masomo ya sayansi, alishinda tuzo hiyo inayotolewa na Raoul Wallenberg Academy kwa kushirikiana na Swedish Institute, kutokana na mchango wake wa kuboresha mazingira ya hedhi salama kwa wasichana kupitia ubunifu wa taulo za hedhi za kufua.
Ubunifu huo umechangia kuboresha afya na mahudhurio ya shuleni kwa wanafunzi wenzake, huku akitoa elimu mwenyewe na kusambaza taulo hizo rafiki kwa mazingira.
Akielezea safari yake, Miriam alisema aliamua kubuni taulo hizo baada ya kupitia changamoto binafsi alipokuwa kidato cha kwanza, hali iliyomsukuma kutafuta suluhisho litakalowanufaisha wasichana wenzake.
Tuzo ya Young Courage Award hutolewa kila mwaka kwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 13 hadi 20, walioonesha ujasiri, ubunifu na mchango chanya katika kubadilisha maisha ya jamii zinazowazunguka.
Kwa mwaka huu, tuzo hizo zimetolewa kwa vijana 12 kutoka mataifa 11 ikiwemo Australia, Canada, Greece, Hungary, Monaco, New Zealand, Norway, Poland, Serbia, Sweden (vijana 2) na Tanzania.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED