CFIT-III inavyosisimua kukabili tatizo la ajira nchini

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 11:12 AM Aug 29 2025
Wadau wa elimu waliokutana katika kikao kazi cha Mradi wa  CFIT III wakiwa katika picha ya pamoja.
Picha: Mpigapicha Wetu
Wadau wa elimu waliokutana katika kikao kazi cha Mradi wa CFIT III wakiwa katika picha ya pamoja.

Uamuzi wa serikali ya Tanzania na wabia wa maendeleo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), kutekeleza Mradi wa China Funds-In-Trust Project Phace-III, unaolenga ‘kusisimua’ maendeleo ya elimu ya juu ya ufundi, ili kujenga nguvu kazi ya kiufundi na bunifu kwa maendeleo ya taifa, umeanza kuonyesha njia ya kukabiliana na tatizo la ajira nchini.

Akizungumza jana Jijini Arusha, wakati wa kikao kazi cha wadau wa elimu, Mhadhiri na Mratibu Msaidizi wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Evaristo Mtitu, amesema moja ya kazi ya mradi huo ni kukuza mbinu za ufundishaji zenye mwelekeo wa soko la ajira, na kuimarisha ujifunzaji unaozingatia uwezo.

Kikao kazi hicho cha siku mbili, kimewahusisha wadau wa elimu, wakiwemo Wahadhiri, Waajiri, na Sekta Binafsi.

Asema kupitia mradi huo wa kuimarisha uwezo za taasisi ya elimu ya juu nchini, wahitimu wa vyuo vya elimu ya juu ya ufundi, wanapata ujuzi na maarifa yanayohitajika kwa soko la ajira na mahitaji ya jamii yanayoendelea. 

Mradi huo wa CFIT III, unafadhiliwa na Serikali ya Watu wa China, na kutekelezwa na UNESCO, unavinufaisha moja kwa moja Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST). 

“Changamoto kubwa inayojitokeza ni wahitimu wengi kushindwa kuendana na uhalisia wa soko la ajira, kwa kushindwa kutumia maarifa yao kwa vitendo, jambo ambalo linawapunguzia ushindani kwenye soko ajira. 

Aidha, mmoja wa wadau wa Mradi wa CFIT III, Charles Ndahani, akichangia mada katika kikao hicho, amesema wanaamini mradi huo unaweza kuwa mwarobaini wa kupungua changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana, hasa kutokana na changamoto ya kushindwa kukidhi mahitaji ya soko la ajira. 

Katika kikao hicho, Mkuu wa Kitengo cha Elimu wa UNESCO, Dk. Faith Shayo, amesema lengo la mradi huo ni kujenga uwezo wa taasisi za elimu ya juu ili kukabiliana na mahitaji ya ujuzi kwa maendeleo ya taifa. 

Madhumuni ya jumla ya CFIT III, ni kuongeza uwezo wa taasisi za elimu ya juu ili kukabiliana na mahitaji ya ujuzi kwa maendeleo ya taifa kwa kuwezesha ushirikiano kati ya taasisi za elimu ya juu na sekta, kuimarisha ufundishaji unaozingatia soko la ajira, na kuimarisha ujifunzaji unaozingatia uwezo.

 Mradi huo wa CFIT III, unakamilisha kikamilifu mageuzi ya elimu yanayofanyika Tanzania, ili kuendeleza Ajenda ya Elimu 2030. 

"Kupitia mradi wa CFIT III, tunakuza ushirikiano kati ya taasisi za elimu ya juu na sekta hiyo, kukuza mbinu za ufundishaji zenye mwelekeo wa soko la ajira, na kuimarisha ujifunzaji unaozingatia uwezo. Hii huwapa wanafunzi ujuzi na maarifa yanayohitajika kwa soko la ajira na mahitaji ya jamii yanayoendelea," amesema.

1