Takribani asilimia 60 ya Watanzania hutumia tiba asili kwa ajili ya kujitibu maradhi mbalimbali, ingawa bado hakuna utafiti unaoeleza kwa kina iwapo watumiaji hao wanatoka mijini au vijijini.
Hayo yamebainishwa leo jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto kutoka Wizara ya Afya, Dk. Ahmad Makuwani, wakati akifungua Kongamano la Nne la Kisayansi la Tiba Asili.
Dk. Makuwani amesema Serikali imetoa kipaumbele kwa tiba asili kutokana na matokeo chanya yaliyoonekana kwa wagonjwa waliotumia mbinu hizo, hasa katika kipindi cha janga la UVIKO-19.
“Katika kipindi cha COVID-19, tiba asili zilionekana kusimama na kutusaidia zaidi, wakati mwingine kuliko dawa za kitaalamu. Labda kinachokosekana hapa ni mifumo ya kirufaa, ambayo kama ingetumika, ingeongeza usalama na ufanisi zaidi,” amesema Dk. Makuwani.
Hata hivyo, amesisitiza umuhimu wa wataalamu kufanya utafiti wa kina badala ya kutegemea simulizi za kiasili ambazo wakati mwingine zinaweza kuchelewesha matibabu au hata kuleta madhara.
Aidha, ameitaka jamii kuendeleza ujuzi wa tiba asili kwa kuwarithisha vijana ili kuimarisha urithi wa maarifa ya tiba za asili na kulinda misitu, kwa kuwa maliasili hizo ndizo chanzo kikuu cha dawa za kiasili.
“Kuwepo kwa maabara zenye ubora kutasaidia kuzalisha dawa salama na bora zaidi, huku vijana wakirithishwa ujuzi huu wataona umuhimu wa misitu na mazao yake,” ameongeza.
Kongamano hilo limekusanya wataalamu wa afya, wanasayansi na wadau mbalimbali kwa lengo la kujadili namna ya kuendeleza tiba asili kwa manufaa ya jamii na maendeleo ya taifa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED