Kitendo cha Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kurasimisha biashara ya usafiri wa bodaboda kuwa sehemu ya usafiri wa umma kimewafanya waendesha bodaboda na bajaji visiwani humo kumchangia fedha za kuchukua fomu ya kugombea tena Urais wa Zanzibar.
Umoja wa Jumuiya ya Waendesha Bodaboda na Bajaji Zanzibar walimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja kiasi cha shilingi 300,000 mchango wao maalum kwa ajili ya Dk. Mwinyi kuchukua fomu hiyo leo, Agosti 30.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Hussein Abushiri Hussein, alisema kurasimishwa kwa biashara ya bodaboda kumewezesha vijana wengi kujiajiri na kujipatia kipato cha kila siku.
Aliongeza kuwa moja ya ahadi kuu alizotoa Dk. Mwinyi wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 ilikuwa ni kurasimisha biashara ya bodaboda, na alitekeleza ahadi hiyo ndani ya muda mfupi baada ya kuingia madarakani.
“Dk. Mwinyi ametufanyia wema mkubwa. Sisi waendesha bodaboda na bajaji tumeamua kumrudishia wema huo kwa mchango huu mdogo tulioukusanya na leo tumemkabidhi,” alisema Mwenyekiti huyo.
Biashara ya bodaboda na bajaji Zanzibar ilirasimishwa rasmi mwaka 2021, hatua ambayo imeendelea kutambuliwa na kupongezwa na wanajamii hususan vijana.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED