MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk. Samia Suluhu Hassan ameahidi kuendelea kuufungua Mkoa wa Kilimanjaro kwa miundombinu ya barabara za lami, zege na changarawe ili kuchochea uchumi.
Dk. Samia ameyaeleza hayo leo Oktoba Mosi, 2025 wakati wa mkutano wa kampeni Moshi Mjini Mkoani Kilimanjaro, akisema miongoni mwa barabara zitazojengwa ni pamoja na ya Holili - Tarakea yenye urefu wa Kilomita 53 ikitajwa kukuza biashara kati ya Tanzania na Kenya, pamoja na kuondoa foleni ya malori kwenye barabara ya Mwika - Tarakea.
Ameahidi pia kuendelea na ujenzi wa barabara ya mchepuko ya Kia Airport yenye urefu wa Kilomita 31 kwa kiwango cha lami, ujenzi wa barabara za ndani ya mji wa Moshi kupitia mradi wa uendelezaji miji Tanzania maarufu kama TACTIC pamoja na kukamilisha barabara ya Moshi International school- Kibosho Kati- Kwa Raphael yenye urefu wa Kilomita 13.
Aidha, Dk. Samia amezungumzia pia ujenzi wa barabara nyingine kwenye Wilaya za Rombo na Moshi Vijijini, akiahidi pia kushughulikia ujenzi wa barabara za viwango vya lami na zege kwenye Wilaya ya Same maeneo ya milimani ili kuzifanya barabara za wilaya hiyo kupitika kwenye msimu ya mvua.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED