Hatari ya maudhui yenye porojo za ngono kwa taifa

By Beatrice Moses , Nipashe
Published at 07:56 PM May 14 2025
Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Wakili Onesmo Olengurumwa
Picha: Beatrice Moses
Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Wakili Onesmo Olengurumwa

MAUDHUI yasiyo na tija hasa porojo zinazohusisha masuala ya ngono na burudani yanayoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini, yametajwa kuwa ni hatari kwa maendeleo kwa ujenzi wa jamii inayofikiri na kuchambua mambo kwa kina.

Aidha vyombo vya habari vimetakiwa kuzingatia wajibu wa kutengeneza ajenda muhimu kwa jamii, kusimamia tasnia na habari za kina kwa kuwa si nyepesi zinazoshinikizwa kuwepo na baadhi ya watu, ili kujifurahisha au kujinufahisha binafsi. 

Hayo yameyasemwa leo Mei 14, 2025 na Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Wakili Onesmo Olengurumwa, wakati akifungua mjadala kuhusu uendelevu wa vyombo vya habari.

Amesema vyombo vya habari vina wajibu mkubwa wa kuikomboa, kuiendeleza jamii kwa kuandika habari zenye maudhui bora yanayoleta matokeo chanya katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla. 

Mjadala huo umeandaliwa na Umoja wa Wachapishaji wa Magazeti Ulimwenguni (WAN-IFRA), kwa kushirikiana na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA TAN) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC).

Olengurumwa amesema licha ya kuwa na vyombo vingi vya habari bado havitimiza wajibu wake vyema wa kutengeneza ajenda na kwamba ni lazima kubadilika kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia.

Mjadala huo umewahusisha baadhi ya wamiliki wa vyombo vya habari Tanzania (MOAT),MISA TAN, Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA).
Mwisho