H’shauri Kigamboni, wadau wageukia upande wa miti

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 07:27 PM Apr 16 2025
Ofisa Misitu kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni, Zaria Msafiri (katikati), akipanda mti katika bonde la Boko, Mtaa wa Mkwajuni, Kata ya Vijibweni, Wilaya ya Kigamboni, mkoani Dar es Salaam. Shirika la Hatua za Wanawake kuelekea kiuchumi (WATED)
Picha: Christina Mwakangale
Ofisa Misitu kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni, Zaria Msafiri (katikati), akipanda mti katika bonde la Boko, Mtaa wa Mkwajuni, Kata ya Vijibweni, Wilaya ya Kigamboni, mkoani Dar es Salaam. Shirika la Hatua za Wanawake kuelekea kiuchumi (WATED)

WAKAZI wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni, Mkoa wa Dar es Salaam wameanzisha mkakati wa upandaji miti, kwa lengo la kukabiliana na mafuriko yanayolikumba eneo hilo.

Ofisa Msaada wa Kisheria wa Shirika la Hatua za Wanawake kuelekea kiuchumi (WATED), Wolflam Kiri, amezungumza hayo jijini Dar es Salaam, wakati wa zoezi hilo, ameeleza umuhimu wa mradi huo.

Amesema juhudi hizo zimejikita katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko kiwa wakati, kwa kuzuia mmomonyoko wa udongo na kuboresha mandhari ya manispaa hiyo.

Ofisa Misitu kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni, Zaria Msafiri (katikati), akipanda mti katika bonde la Boko, Mtaa wa Mkwajuni, Kata ya Vijibweni, Wilaya ya Kigamboni, mkoani Dar es Salaam. Shirika la Hatua za Wanawake kuelekea kiuchumi (WATED), imeshirikiana na halmashauri hiyo kupanda miti 70 eneo hilo, ili kuzuia mmomonyoko wa udongo
“Kampeni hiyo inayoongozwa WATED, ilizinduliwa eneo la Boko Bwawani, Mtaa wa Mkwajuni ndani ya Kata ya Vijibweni. Tumeanza kupanda miche ya miti 70 katika eneo la Boko Bwawani, ili kupambana na mmomonyoko wa udongo,” amesema.

Pia ameongeza kuwa, hatua hiyo itapunguza hatari ya mafuriko na maporomoko, madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwa kuhamasisha upandaji wa miti kwa jamii. 

“Eneo hili limekuwa likikumbwa na athari kubwa hasa msimu wa mvua, hivyo mbali na kujengwa miundombinu bado miti ni suluhisho,” amesema.

Amesema upandaji huo, umeshirikisha wakazi wa eneo hilo, viongozi wa Mtaa wa Mkwajuni, maofisa kutoka halmashauri hiyo, wanachama wa Shirika la Tanzania Youth Behavioural Change Organization (TAYOBECO).

“Kutokana na mafuriko ya mara kwa mara, baadhi ya wakazi tayari wamelazimika kuhama baada ya serikali kutoa agizo la kuhama maeneo hatarishi. Tunatoa wito kwa jamii kutunza na kulinda miti hii mipya tuliyopanda. 

“Rasilimali zimewekezwa kununua miche hii kwa ajili ya kusaidia maeneo haya yaliyoathiriwa na mafuriko,” alisema Kiri.

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Julita Joseph, alisifu juhudi hizo na kusisitiza jinsi WATED na washirika wake wanavyochukua kwa uzito changamoto za kimazingira.

“Wakati mvua inaponyesha, maji hukusanyika na kutuama katika eneo hili kwa sababu wakandarasi waliotengeneza mifereji ya kupitisha maji walielekeza maji kuja kwenye makazi yetu badala ya kuelekeza baharini,” ameeleza.

Ofisa Ushirikishaji wa TAYOBECO, Rodrick Massawe, amesema shirika lao limejiunga na kampeni hiyo ili kusaidia kulinda mazingira na kuboresha ustawi wa jamii kwa kuhamasisha hewa safi, vivuli vya asili na mandhari yenye mvuto zaidi.

Ofisa Misitu kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni, Zaria Msafiri, amesema hatua hiyo itaokoa mazingira ambayo kila wakati wa mvua huathiriwa.