Shura ya Maimamu yatoa rai , marekebisho dosari za uchaguzi

By Imani Nathaniel , Nipashe
Published at 01:25 PM Jun 07 2025
Katibu Mkuu wa Shura ya Maimamu Nchini Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda akisoma taarifa kuhusu uchaguzi ujao.
PICHA: IMANI NATHANIEL
Katibu Mkuu wa Shura ya Maimamu Nchini Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda akisoma taarifa kuhusu uchaguzi ujao.

Shura ya Maimamu Tanzania imetoa waraka wa Idd Adh-aa wakiwataka waislamu kushiriki uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu,na kuitaka serikali kuboresha huduma za afya na mifumo ya uchaguzi.

Aidha, imesema ni muhimu uchaguzi ukawa wa haki, sheria bora, elimu yenye tija, na huduma bora kwa wananchi wote kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025. Katika taarifa hiyo iliyosomwa leo Mei 7, 2025 na Katibu Mkuu wa Shura ya Maimamu Nchini Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, amesema kuwa uchaguzi nchini zimekuwa na kasoro kubwa, ikiwemo matumizi ya nguvu, uminywaji wa haki za wagombea na ukiukwaji wa demokrasia, hali inayohatarisha amani ya nchi.

“Uchaguzi wa 2025 unaweza kuwa wa amani kabisa, ikiwa serikali itashirikiana na wadau kupitia majadiliano ya wazi na marekebisho ya sheria za uchaguzi. amesema Ponda.Aidha,viongozi hao wameitaka serikali kupitia upya Sheria ya Uchaguzi, Sheria ya Vyama vya Siasa, na sheria zinazohusu Jeshi la Polisi kwa kushirikisha wadau mbalimbali kabla ya uchaguzi.

Pia, wamependekeza kuwepo kwa kikao maalum cha tathmini ya amani ya uchaguzi ndani ya siku 30 kabla ya kupiga kura, na kwamba makubaliano yake yaheshimiwe na vyombo vyote vya dola. Wamesisitiza kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwamba inapaswa kutenda haki kwa wagombea wote, kuhakikisha uwazi katika kila hatua ya uchaguzi, na kutangaza mshindi kwa mujibu wa ridhaa ya wananchi bila urasimu au upendeleo.

Aidha, imevitaka vyombo vya ulinzi na usalama vimetakiwa kujifunza kutoka kwenye matukio ya nyuma ili kuepuka lawama na matukio ya uvunjifu wa amani, utekaji au mauaji kama ilivyowahi kuripotiwa katika baadhi ya chaguzi zilizopita.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa licha ya zaidi ya miaka 60 ya uhuru, Tanzania bado inakabiliwa na changamoto za umasikini mkubwa. Imetoa mapendekezo ya haraka kama vile kupunguza kodi kwenye bidhaa muhimu, kuajiri vijana waliokosa ajira, na kufanya tathmini ya sera na mifumo ya kiutendaji kwa kutumia taasisi huru ili kubaini vikwazo halisi vya maendeleo.