KATIBU Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma(CHAUMMA), Salum Mwalimu, amewaomba wale wenye nafasi ya kuhimiza amani ya nchi, watumie nafasi hiyo pia kuhimiza kutendeka kwa haki katika uchaguzi mkuu mwaka huu.
Amewataka wenye Mamlaka ya kusimamia uchaguzi mkuu mwaka huu, kutenda haki kwa kuhakikisha uchaguzi huo unakuwa huru, haki na wa kuaminika. Salumu Mwalimu amesema hayo leo alipoungana na waumini wa dini ya Kiislam katika Msikiti wa Bakwata- Masjid Noor, Bariadi mkoani Simiyu, kuswali swala ya Eid.
"Tutaihubiri amani, lakini tutaihubiri na haki kwao wanaohusika kusimamia uchaguzi ili uwe mzuri, tumalize tukiwa wamoja, tukiwa watu ambao tuko tayari kuiendeleza Tanzania yetu." Amewaomba wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo kwa kujitokeza kugombea na kupiga kura.
"Chagueni viongozi ambao watasimamia maendeleo yenu, nendeni na ninyi mkagombee, hakuna kujiweka nyuma," amesema Salum Mwalimu. Shekhe wa mkoa wa Simiyu, Issa Kwezi, amewataka Watanzania kutokukubali kutumika kuchafua na kuharibu amani ya nchi.
"Kibaya zaidi viongozi wa dini tunaposisitiza jambo kama hili, tunaonekana tuko upande fulani. Lakini tukumbuke kuwa amani ikiharibika, hakuna mtu atakayesalimika. "Ikishaondoka amani, kila mmoja atabaki analia na kuilaumu nafsi yake,"amesema Shekhe Kwezi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED